HALI YA KUTISHA, MTO WA PWANI YAONGOZA UKATAJI WA MIKOKO KASKAZINI UNGUJA
NA ABDUL SAKAZA
Shehia Ya Mto
Wa Pwani imetajwa kuongoza kwa ukataji na uharibifu wa Mikoko Mkoa Wa Kaskazini
Unguja, ikifuatiwa na Tumbatu, huku Muawada ikishika nafasi ya tatu.
Kwa upande
mwingine, Shehia ya Kiongwe Kidogo imetajwa kuwa kinara wa uhifadhi wa Mikoko
kwa kutokata misitu hiyo na kuwa mfano wa kuigwa katika juhudi za uhifadhi wa Mazingira
ya Pwani Mkoani humo.
Taarifa
hiyo imetolewa na Afisa Misitu Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Sleyum Saidi Khamis,
wakati akizungumza na mwandishi wa habari wa Sakaza Digital mapema wiki hii ambapo
amesema kwa mwaka 2025 jumla ya mikoko 5,050 imekatwa katika shehia za Mto wa
Pwani, Tumbatu na Muawada.
Kulingana
na taarifa hiyo, Mto wa Pwani inaongoza kwa kukatwa mikoko 2,900, ikifuatiwa na
Tumbatu mikoko 1,200, huku Muawada ikirekodi mikoko 950 iliyokatwa.
Amesema
licha ya kiwango hicho cha uharibifu, Serikali kwa kushirikiana na vikundi vya
uhifadhi na wadau wa mazingira imefanikiwa kupanda jumla ya mikoko elfu nane(8,000)
katika shehia za Tumbatu, Muawada, Bumbwini, Kiongwe Kidogo, Fujoni na Mto wa
Pwani, kama sehemu ya mkakati wa kufidia mikoko iliyoharibiwa na kukabiliana na
athari za mabadiliko ya tabianchi.
Afisa huyo
pia amesema ingawa juhudi za upandaji wa
mikoko zinaendelea, bado changamoto ya ukataji wa mikoko kwa ajili ya kuni na
ujenzi inaendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo hali inayohitaji
ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na jamii.
Kunaathari
Gani Kukata Mikoko Kisiwani Tumbatu?
Dokta
Sharif Alawi Badru ni Mtaalamu wa Mazingira na Majanga ya Asili kutoka Mombasa
Nchini Kenya ameweka bayana kua kukata mikoko katika maeneo ya visiwa kama vile
Tumbatu kunaweza kusababisha kutokea majanga asili kama vile upepo mkali wenye
madhara ,kupanda kwa kina cha maji ya
Bahari katika makaazi ya watu na mmong’onyoko wa aridhi.
“Kukata
mikoko Tumbatu ni hatari sana. Upepo unapovuma unaingia moja kwa moja katika
makazi ya watu, na ndiyo maana Tumbatu imekuwa ikiathiriwa mara kwa mara, kwa
sababu mikoko ambayo ni kizuizi cha asili cha upepo inaendelea kukatwa,” aliesema.
Ameongeza
kuwa mikoko ni ngao muhimu dhidi ya mmomonyoko wa ardhi na mawimbi makali ya
bahari, hivyo kuendelea kuharibiwa kunahatarisha makazi, mashamba na
miundombinu ya kijamii ya wakazi wa kisiwa hicho.
Aidha,
ukataji wa mikoko Tumbatu unasababisha kupungua kwa mazalia ya samaki, hali
inayowaathiri moja kwa moja wavuvi na wananchi wanaotegemea bahari kwa kipato
na chakula, jambo linaloathiri ustawi wa uchumi wa jamii hiyo
Kwa Nini
Mikoko Mto wa Pwani Inakatwa
Mbarouk
Khamis Zahor ni Mwenyekiti wa Kikundi
cha Hifadhi ya Bahari Mto wa Pwani, Akizungumzia suala la ukataji wa mikoko katika
Shehia hiyo amekiri kuwepo kwa
changamoto hiyo licha ya jitihada za uhifadhi na upandaji wa mikoko zinazofanywa na kikundi chao.
“Ni kweli
changamoto bado ipo. Licha ya jitihada zetu, zaidi ya mikoko 2,900 imekatwa Mto
wa Pwani,” amesema Mbarouk.
Amesema
mikoko hiyo hukatwa zaidi na wananchi kutoka maeneo jirani ya Mkokotoni na
maeneo mengine kwa ajili ya shughuli za
ujenzi na matumizi ya kuni, hali inayochangia kuendelea kwa uharibifu wa misitu
hiyo muhimu ya pwani.
Mbarouk
amesema kwa sasa kikundi cha hifadhi ya Bahari , kwa kushirikiana na viongozi
wa shehia, kimeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha hakuna nyumba wala
vibanda vinavyojengwa kwa kutumia mti wa mikoko.
“Tumeamua
kusimamia kwa ukali matumizi ya mikoko ili kuzuia uharibifu zaidi,”
ameongeza.
Amesema
juhudi hizo zinaambatana na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa
mikoko katika kulinda fukwe dhidi ya mmomonyoko wa ardhi, kuhifadhi mazalia ya
viumbe wa baharini na kuimarisha maisha ya wananchi wanaotegemea uvuvi.
Wanawake Wa
Mto Wapwani Wanaathirika Vip Na Ukataji Wa Mikoko
Bii Mwanaidi Hamad (60), mkazi wa
Mto wa Pwani ni Katibu wa Kikundi cha
Hifadhi ya Bahari, amesema ukataji wa mikoko unaathiri kwa kiwango kikubwa
maisha ya wanawake wa eneo hilo kwani kupitia kikundi hicho huweka makusanyo ya
fedha ambayo huwasadia kukopeshana ili kukidhi mahitaji yao ya kimaisha.
“Mikoko ni chanzo cha maisha
yetu. Unapokata mikoko unawaathiri wanawake moja kwa moja na unarejesha nyuma
juhudi zetu za kujikimu kimaisha,” amesema.
Kando na hilo Semeni Dadi Haji ni
mjumbe wa kikundi hicho amewaomba wanaojihusisha na suala la ukataji wa Mikoko
katika Shehia Ya Mto Wa Pwani kuacha
maramoja ili kutimiza ndoto za wanawake za kujikwamua na umasikini kupitia
mikoko na wamewaomba wahisani kuwapatia vitendea kazi vinavyohitajika ili kuendelea kuhifadhi na upandaji wa
Mikoko.
Kwa upande wake,
Sheha wa Shehia ya Mto wa Pwani, Moh’d Ali Ali, amesema uongozi wa shehia
unatambua juhudi za kikundi cha hifadhi ya Bahari na umekuwa ukishirikiana nao katika kila hatua
ya kupanda, kutunza na kuhifadhi mikoko, kama mkakati wa kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi.
Pia amepongeza
juhudi za wananchi wa Kiongwe Kidogo kwa kuonyesha uelewa na uzingatiaji wa
sheria za uhifadhi wa mazingira huku akitumia mfano huo kuwataka wananchi wa shehia yake kuiga mfano
huo


.jpeg)

No comments