SHERIA MPYA YA HABARI YANUKIA ZANZIBAR
NA FATMA RAJAB
WIZARA ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo imesema kuwa mchakato wa kuandaa sheria mpya ya habari unaendelea vizuri na utakamilika hivi karibuni ili kufikishwa katika Baraza la Wawakilishi kuendelea na hatua zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Ali Abdul-Gulam Hussein, alipokuwa akifunga semina ya siku moja iliyowashirikisha wadau wa vyombo vya habari Zanzibar, iliyofanyika katika ukumbi wa ZURA.
Alisema serikali imejipanga kuhakikisha sheria hiyo mpya inakidhi mahitaji ya wakati uliopo, sambamba na kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na ukuaji wa sekta ya habari.
Alieleza kuwa sheria iliyopo sasa yazamani, hali inayochangia kuwepo kwa changamoto katika utendaji wa vyombo vya habari na wadau wake.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa mchakato huo kutasaidia kuweka mazingira bora zaidi ya kazi kwa wanahabari pamoja na kuimarisha uwajibikaji na taaluma ndani ya sekta hiyo.
Aidha, alifahamisha kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta ya habari katika maendeleo ya jamii, hususan katika kutoa elimu, kuhabarisha na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Alisema kuwa kutokana na umuhimu huo, serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha sekta hiyo inakuwa imara na yenye kuzingatia maadili ya taaluma.
Alifafanua kuwa mchakato wa sheria hiyo umehusisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha unakuwa jumuishi na unaoakisi mahitaji halisi ya sekta ya habari nchini.
Hivyo aliwataka wadau wa vyombo vya habari kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kukamilisha hatua zilizobaki za maandalizi ya sheria hiyo muhimu.
“Tunatambua matarajio yenu na umuhimu wa sheria hii, hivyo tunaomba muendelee kuwa wavumilivu wakati taratibu hizi zinakamilishwa kwa manufaa ya sekta nzima,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Hiji Shajak, alisema kuwa semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo wadau wa habari kuhusu masuala ya kitaaluma na mabadiliko ya sekta hiyo.
Alifahamisha kuwa ni muhimu kwa wanahabari kuendelea kujifunza na kujiboresha ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya jamii.
Washiriki wa semina hiyo walieleza kuwa wamefaidika kwa kiasi kikubwa na mafunzo hayo, wakisema yamewapa uelewa mpana juu ya masuala ya kisheria na kitaaluma katika tasnia ya habari.
Walisema kuwa semina hiyo imewasaidia kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili na kujadili namna bora ya kuzitatua kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine.
Semina hiyo ya siku moja kwa watendaji wa vyombo vya habari imeandaliwa na Tume ya Utangazaji Zanzibar ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya habari nchini

No comments