Breaking News

WAHASIBU NA MAOFISA MIPANGO WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA TA TAALUMA ZAO



Na Said Khamis.

 OFISI ya Msajili wa Hazina Zanzibar imewataka wahasibu na maofisa mipango wa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha wanazingatia taaluma, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali katika mchakato mzima wa uandaaji na utekelezaji wa bajeti.

 

Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo maalum ya uandaaji wa bajeti yaliyowakutanisha wahasibu na maafisa mipango kutoka taasisi mbalimbali za umma, yakilenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha za serikali.

 

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mipango kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sleyum Abdallah Juma, alisema kuwa ni muhimu kwa watendaji hao kuelewa kikamilifu mchakato wa bajeti ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa tija.

 

Alifahamisha kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha usimamizi wa fedha, ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo watendaji wake kupitia mafunzo ya mara kwa mara.

 

Alisema kuwa bajeti bora ni msingi wa utekelezaji mzuri wa mipango ya maendeleo, hivyo ni lazima iandaliwe kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa pamoja na mahitaji halisi ya taasisi husika.

 

Kwa upande wake, Ofisa Mipango kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar, Abdallah Salum Abdallah, aliwataka washiriki kutumia ipasavyo maarifa waliyoyapata ili kuboresha utendaji wao wa kazi za kila siku.

 

Alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watendaji katika uandaaji sahihi wa bajeti, usimamizi wake pamoja na utekelezaji wake kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa.

 

Aidha, alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza makosa yanayojitokeza katika upangaji wa bajeti na kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za umma.

 

Aliongeza kuwa kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika uandaaji wa bajeti, ikiwemo changamoto za kimfumo ambazo zimekuwa zikichangia kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo.

 

“Ni muhimu kwa watendaji wote kuelewa kwa kina mchakato mzima wa uandaaji wa bajeti ili kuhakikisha rasilimali za serikali zinapangwa na kutumika kwa tija na uwajibikaji,” alisema Abdallah.

 

Alisisitiza kuwa kila mshiriki anawajibika kutumia maarifa aliyoyapata kuboresha mipango ya taasisi zake na kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.

 

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu mbinu bora za uandaaji na usimamizi wa bajeti.

Walisema mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya wa namna ya kukabiliana na changamoto walizokuwa wakizipata katika kazi zao za kila siku.

 

Walibainisha kuwa elimu hiyo itasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma, hali itakayochangia kuimarika kwa utendaji wa taasisi zao.

 

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha na kuhakikisha kunakuwa na usimamizi bora wa rasilimali za umma.

 

Hatua hiyo pia inalenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo na hatimaye kuchochea ustawi wa wananchi pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

 


No comments