Breaking News

RIPOTI YA HAKI ZA BINADAMU 2025 KUCHOCHEA MABORESHO YA SERA ZANZIBAR



Na Siti Ali.

Wadau wa haki za binadamu Zanzibar wamesema kukamilika kwa ripoti ya haki za binadamu kwa mwaka 2025 kutakuwa chachu muhimu ya kuboresha sera, sheria na utoaji wa huduma kwa wananchi, hatua itakayochangia kuimarisha ustawi wa jamii. Kauli hiyo ilitolewa wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya awali ya utafiti huo kwa wadau mbalimbali visiwani humo.

Mshauri Mwelekezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Castor Kalemera, alisema utafiti huo unalenga kukusanya na kuhakiki maoni ya wananchi kuhusu hali halisi ya haki za binadamu Zanzibar. Alieleza kuwa zoezi hilo linaendeleza utafiti kama huo uliofanyika mwaka 2024 na kwamba matokeo yake yatatoa picha sahihi ya mafanikio yaliyofikiwa pamoja na changamoto zilizopo.

Alifafanua kuwa utafiti huo umeangazia kwa kina nyanja mbalimbali za haki za binadamu, ikiwemo haki za kijamii na kisiasa, haki za kiuchumi na kiutamaduni, pamoja na haki za maendeleo. Aidha, umechunguza ushiriki wa Wazanzibari katika mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii na fursa zinazotokana na utamaduni na uchumi wa buluu.

Kalemera alibainisha kuwa haki za makundi maalum, hususan watu wenye ulemavu, zimezingatiwa katika utafiti huo, huku akieleza kuwa bado kuna changamoto ikiwemo matumizi duni ya lugha ya alama katika baadhi ya huduma. Hata hivyo, alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto hizo.

Akizungumzia mafanikio, alisema ripoti ya mwaka 2024 imechangia kupungua kwa matukio ya ukatili wa kijinsia mwaka 2025, jambo linaloonesha umuhimu wa tafiti hizo katika kuleta mabadiliko chanya. Alitoa wito kwa wadau kutumia matokeo ya ripoti hiyo kupanga mipango ya maendeleo na kuongeza uelewa wa haki na wajibu kwa wananchi.

Kwa upande wao, baadhi ya wadau wakiwemo Inspekta wa Polisi Sadiki Ali Sultan na Shumbana Abdulhakim Muhsin, walisema utafiti huo utasaidia kubaini mapungufu katika utoaji wa huduma, hususan maeneo ya vijijini. Mkutano huo uliandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), huku ripoti kamili ikitarajiwa kutolewa baadaye mwaka huu.


No comments