Na Juma Seif.
Masheha katika kisiwa cha Pemba wamehimizwa kutumia ipasavyo vishkwambi walivyokabidhiwa ili viwasaidie kuboresha utendaji wao wa kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi. Wito huo umetolewa na viongozi mbalimbali wa serikali wakisisitiza kuwa matumizi sahihi ya teknolojia yataongeza ufanisi katika ngazi ya shehia na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa jamii.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia, Habari na Ubunifu, Moh’d Sijiamin Moh’d, amesema kuwa katika dunia ya sasa mambo mengi yanafanyika kwa njia ya kidijitali, hivyo ni muhimu kwa Masheha kwenda sambamba na mabadiliko hayo. Ameeleza kuwa vishkwambi hivyo vitasaidia wananchi kuwasiliana kwa urahisi na ofisi za Masheha kupitia mitandao bila kulazimika kufika moja kwa moja ofisini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Hawwah Ibrahim Baye, amesema mpango huo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linalolenga kuimarisha matumizi ya teknolojia katiaka utoaji wa huduma za umma. Ameongeza kuwa hatua ya awali imeanza katika ngazi ya jamii ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa karibu zaidi.
Mapema, Kaimu Afisa Mdhamini wa wizara hiyo, Ibrahim Saleh Juma, ameeleza kuwa serikali itaendelea kufuatilia matumizi ya vifaa hivyo ili kuhakikisha vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Amebainisha kuwa elimu kwa watumiaji itaendelea kutolewa ili kuongeza uelewa na ufanisi katika matumizi ya teknolojia hiyo.
Nao baadhi ya Masheha wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo wakisema itawarahisishia kazi zao za kila siku, hasa katika kuhifadhi taarifa na kumbukumbu muhimu za wananchi. Wamesema matumizi ya vishkwambi yataongeza kasi ya utendaji kazi na kupunguza changamoto zilizokuwepo hapo awali.
Sheha wa Tumbe Magharibi, Masoud Khamis Hamad, pamoja na Sheha wa Shehia ya Uweleni, Abdalla Omar Mjawiri, wameahidi kutumia vifaa hivyo kwa ufanisi mkubwa ili kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha wanakwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia kwa manufaa ya jamii.A
No comments