Breaking News

WAZAZI, WALEZI , NA WALIMU WAASWA KUSHIRIKIANA MALEZI YA WATOTO.

 


Na: Nishan Khamis, Moga

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa karibu na walimu wa madrasa na skuli katika malezi ya watoto ili wakue katika maadili mema sambamba na kuepukana na vitendo vya udhalilishaji.

Waziri Riziki ameyasema hayo leo katika kijiji cha Moga, Mwembe Mkali, Wadi ya Kidombo, Jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A alipokuwa mgeni rasmi katika Maulid ya Maadhimisho ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na Madrasa ya Ikram Muslimina.

Aidha, ametoa pongezi kwa walimu wa madrasa hiyo kwa juhudi zao katika ufundishaji wa elimu ya dini sambamba na lugha za kigeni wanazofundishwa wanafunzi hao. Amesema dunia ya sasa ni ya utandawazi na uchumi wa ushindani, hivyo kufundisha lugha za kigeni ni njia mojawapo ya kuwaandaa watoto hao kwa fursa za ajira na kujiajiri.



Katika hatua nyingine, Waziri Riziki ameahidi kusaidia mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya ujenzi unaoendelea katika madrasa hiyo. Pia ameahidi kulifikisha suala la changamoto ya barabara kwa Waziri husika ili lifanyiwe kazi, sambamba na kushirikiana na viongozi wa jimbo hilo kutafuta ufumbuzi wa changamoto nyingine kwa lengo la kuendeleza maendeleo ya dini nchini.

Halikadhalika, ametumia nafasi hiyo kuwanasihi wazazi na jamii kwa ujumla kuendelea kutunza amani na utulivu, kuiombea nchi pamoja na viongozi wake, na kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kwa upande wao, Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A Nyange Kher Ali, pamoja na Diwani wa Wadi ya Kidombo, Makame Machano Fumu, wamesema wamefurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na walimu na wanafunzi wa madrasa hiyo, jambo linalochangia watoto kukua katika maadili mema. Wamesema kazi hiyo inastahili pongezi kwa kuwa ni mchango muhimu katika maendeleo ya dini na taifa kwa ujumla.

Aidha, viongozi hao wamesema wamezipokea changamoto zilizowasilishwa, ikiwemo ubovu wa barabara na mikopo ya uwezeshaji kwa wajasiriamali, na kuahidi kuzifikisha katika mamlaka husika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.



Awali, akisoma risala katika Maulid hayo, mwanafunzi wa madrasa hiyo, Wahda Omar Nyasa, amesema pamoja na mafanikio ya kuibua vipaji mbalimbali kwa wanafunzi, madrasa hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ubovu wa barabara, upungufu wa feni, vifaa vya vyoo, chanarini, saruji pamoja na milango.q


No comments