SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KUWAJENGEA WANAFUNZI MAZINGIRA BORA YA KUJIFUNZIA.
Na Said Khamis.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwajengea wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia kwa kuwawekea dakhalia, hatua itakayowawezesha kujisomea kwa utulivu na kuongeza ufaulu wao.
Dkt. Shein ameyasema hayo leo huko Dole, katika Skuli ya Sekondari Mikindani, wakati wa ufunguzi wa dakhalia za Skuli za Sekondari Lumumba, Misufini na Paje Mtule, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema dakhalia ni nyenzo muhimu katika kuinua taaluma ya wanafunzi kwani huwapatia muda wa ziada wa kujisomea katika mazingira tulivu, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya ufaulu wao.
“Kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, dakhalia zilikuwa chache na zilihudumia wanafunzi wachache waliotoka maeneo ya mashamba, huku wanafunzi wa mjini wakikaa majumbani,” alisema Dkt. Shein.
Ameeleza kuwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, Hayati Jemedari wa Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alitangaza fursa ya elimu bure kwa wananchi wote wa Zanzibar bila ubaguzi wowote.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar amesema ujenzi wa dakhalia hizo ulianza mwezi Septemba 2024 na kukamilika mwezi Desemba 2025.
Amefafanua kuwa mradi wa dakhalia za Skuli ya Sekondari Mikindani unahusisha ujenzi wa dakhalia mbili moja ya wanafunzi wa kike na nyingine ya wanafunzi wa kiume pamoja na jengo la mkahawa wa kisasa unaotumia nishati ya gesi.
Kwa upande wa Skuli ya Sekondari Lumumba, amesema jengo lililojengwa ni dakhalia ya wanafunzi wa kike pekee, kutokana na dakhalia ya wanafunzi wa kiume kujengwa miaka mitatu iliyopita.
Katibu Mkuu huyo amewataka wanafunzi kuzitumia ipasavyo dakhalia hizo kwa lengo la kuimarisha taaluma zao.
Jumla ya Shilingi Bilioni 1.5 zimetumika kutekeleza mradi huo wa ujenzi kwa mujibu wa mkataba.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Amani na Umoja ni Msingi wa Maendeleo Yetu.”


No comments