BARAZA LA SANAA NA MAMLAKA YA MJI MKONGWE LAKEMEA VIKALI TUKIO LA FASION SHOW.
Na Said Khamis.
Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu Zanzibar (BASSFU) Juma Choum Juma amesema kuwa Baraza la Sanaa Zanzibar kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe zinakemea vikali tukio la Fashion Show lililoandaliwa na Kampuni ya Run Awaybay, jambo ambalo ni kinyume na masharti ya kibali walichopatiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara Habari Maelezo Zanzibar Mkoa wa Mjini Magharibi amesema kuwa mamlaka hizo zitachukua hatua dhidi ya tukio hilo.
Amesema tukio hilo lilifanyika kinyume na masharti ya kibali ambapo Kampuni ya Run Awaybay iliruhusiwa kuandaa Maonyesho ya mavazi (Fashion Show) inayohusisha mavazi ya asili ya utamaduni wa Mzanzibar kwa kuzingatia maadili, utamaduni, mila na heshima ya Mji Mkongwe kama eneo la urithi wa dunia.
Amefahamisha kuwa maudhui na muonekano wa maonyesho hayo hayakuwiana na lengo, masharti wala miongozo iliyotolewa, jambo ambalo linakiuka taratibu za kisheria, kiutamaduni na kiuhifadhi zinazolinda hadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Katibu Choum ameeleza kuwa kutokana na ukiukwaji huo, Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa Zanzibar, zimefikia maamuzi na kuchukua hatua ikiwemo
"Tutafanya tathmini upya ya vikundi vyote vya Zanzibar vinavyojihusisha na shughuli za Fashion Show, kwa lengo la kubaini uhalali wao, mwelekeo wa kazi zao na uzingatiaji wa maadili, utamaduni na sheria" alieleza.
Amefafanua kuwa Mamlaka na Baraza zitatengeneza mkakati kambambe wa usimamizi, usaili na usajili, ili kuhakikisha vikundi vyote vinavyofanya shughuli za Fashion Show vinafuata kikamilifu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sanaa, burudani na uhifadhi wa urithi wa Zanzibar.
Alibainisha kuwa Kampuni ya Run Away inaweza kufutiwa na kuondolewa rasmi ruhusa ya kufanya na kushiriki shughuli zote za Fashion Show na matasha yanayohusiana na sanaa ya mavazi ndani ya Zanzibar, kutokana na kukiuka masharti ya kibali na miongozo ya kisheria na kiutamaduni.



No comments