LENGO LA MAPINDIZI NI KUIMARISHA UCHUMI NA JAMII. MH. HEMED SULEIMAN.
Na Siti Ali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema adhma ya kufanyika kwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ni kuimarisha maendeleo katika Sekta zote za kiuchumi na kijamii.
Ameyasema hayo katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi katika jengo la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali lililopo Wilaya ya Chake Chake Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema jengo hilo litawawezesha watumishi wa Wizara ya elimu kufanya kazi zao katika mazingira bora, salama na yanayochochea ubunifu na uwajibikaji.
Mhe. Hemed amesema hadi kufikia mwezi Disemba 2025, Madarasa zaidi ya elf 4 yamejengwa Zanzibar ikijumuisha na ujenzi skuli za ghorofa ambapo Mkoa wa kusini Pemba ni wanufaika wa miradi hio.
Aidha, amefahamisha kuwa Serikali imejipanga kujenga skuli nyengine 29 za ghorofa ambapo zitakwenda kumaliza changamoto katika sekta ya elimu Zanzibar.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameuagiza Uongozi wa Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha wanaweka thamani mpya katika jengo hilo zenye viwango vitakavyodumu kwa muda mrefu na vyenye kukidhi mahitaji ya watumiaji wa jengo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemuelekeza Mkandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa mradi huo kuhakikisha mradi huo unajengwa kwa viwango vinavyotakiwa, kuzingatia muda na thamani ya fedha ambapo Serikali na wananchi wanatarajia kuona matokeo chanya ya mradi huu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Khadija Salum Ali amesema sababu kubwa ya kujengwa kwa jengo hilo ni kuondoa changamoto ya kukodi majengo kwa ajili ya matumizi ya Ofisi lakini pia kuondoa changamoto ya uhaba wa ofisi unaopelekea watendaji wa vitengo tofauti kufanya kazi ndani ya ofisi moja jambo nilokwamisha ufanisi wa utendaji wa kazi.
Mhe. Khadija amewataka vijana kuisoma historia ta nchi yao ili wapate kuyaelewa vyema Mapinduzi matukufu ya zanzibar kuyajua lengo lake ili wapate kuyaenzi na kuyadumisha kwa vitendo mapinduzi hayo.
Akisoma taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa mradi ya Afisi ya Wizara ya elimu Chake Chake, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ndugu Khamis Abdalla Said amesema litakapokamilika jengo hilo litatua changamoto ya ufinyu wa nafasi kwa wafanyakazi wa Wizara jambo litakalotoa msukumo wa kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Katibu Khamisi amesema amepokea agizo la Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar la kutowapa kazi Kampuni ya OSAJU hadi watakapo kamilisha ujenzi wa Jengo hilo na kujiridhisha kuwa wataheshimu na kuthamini makubaliano ya mikataba wanayoweka na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusuni Pemba Ndugu Rashid Hadid Rashid amesema Sekta ya elimu katika Mkoa wa Kusini Pemba imeimarika maradufu kutokana na kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Rais Dkt. Mwinyi kama vile ujenzi wa skuli za ghorofa, dakhalia na ujenzi wa Afisi ya wizara ya elimu Pemba.
Hadid amefahamisha kuwa utakapokamilika mradi wa ofisi ta Wizara ya elimu Pemba utatoa nafasi kwa wafanyakazi kufanya kazi zao katika mazingira mazuri na salama ambayo yataboresha ufanyaji kazi kwa ufanisi na kukuza kiwango cha elimu ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba.
.jpeg)
.jpeg)
No comments