Breaking News

Hali Mbaya ya Hewa Yasitisha Safari za Air Tanzania Kati ya Dar es Salaam na Mbeya



Na Said Khamis.

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imelazimika kusitisha kwa muda safari zake mbili kati ya Dar es Salaam na Mbeya baada ya kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Songwe kutokana na hali mbaya ya hewa iliyokuwepo usiku wa tarehe 04 Januari 2026.

Kwa mujibu wa taarifa ya ATCL iliyotolewa leo Januari 5, 2026, ndege hizo zilizokumbwa na changamoto hiyo ni TC 106 (Airbus A220-300) iliyokuwa imebeba abiria 119, pamoja na TC 2106 (De Havilland Q400) yenye abiria 62. Ndege hizo ziliondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) majira ya saa 2:08 na 2:15 usiku mtawalia, zikiwa na lengo la kutua Mbeya.

Hata hivyo, kutokana na hali ya hewa kutoruhusu kutua kwa usalama katika Uwanja wa Ndege wa Songwe, marubani walichukua uamuzi wa kurejea Dar es Salaam, kwa kuzingatia kikamilifu taratibu na viwango vya usalama wa anga. Hatua hiyo ilihakikisha usalama wa abiria wote, ambao walirejeshwa salama bila madhara yoyote.

ATCL, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), iliendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali ya hewa ili kuona uwezekano wa kuendelea na safari hizo. Licha ya jitihada hizo, hali ya hewa haikuboreka kwa kiwango kilichoruhusu safari kuendelea kwa usalama katika kipindi chote cha usiku, hali iliyosababisha abiria kushindwa kusafiri kwa zaidi ya saa kumi.

Katika kipindi hicho cha kusubiri, ATCL ilihakikisha abiria wote waliokuwa Uwanja wa Ndege wa Songwe (waliopaswa kusafiri na TC 107 na TC 2107) pamoja na wale waliorejeshwa JNIA wanapata huduma muhimu kwa mujibu wa taratibu za Kampuni, ikiwemo huduma za msingi wakati wa kusubiri taarifa zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa za awali kuhusu uwezekano wa kuboreka kwa hali ya hewa, ATCL ilieleza kuwa inatarajia kurejesha safari hizo kwa kuondoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya kabla ya saa 6:00 mchana, na safari ya kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam kabla ya saa 8:00 mchana, endapo hali ya hewa itaendelea kuimarika.

Kampuni ya Air Tanzania imeomba radhi kwa usumbufu uliowakumba abiria wake na imewashukuru kwa uvumilivu wao. Aidha, imesisitiza kuwa usalama wa abiria na wafanyakazi wake utaendelea kuwa kipaumbele kikuu katika utekelezaji wa safari zake zote.


No comments