Breaking News

WATUMISHI WA AFYA WAASWA KULINDA TAALUMA, MAADILI NA WELEDI WA KAZI.

 


OWM-TAMISEMI,Tabora

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, amesema kada ya Afya ni kada maalumu inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi, hivyo watumishi wa sekta hiyo wanapaswa kuilinda kwa wivu mkubwa kwa kuzingatia maadili, weledi na miiko ya taaluma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Prof. Nagu ameyasema hayo alipotembelea hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya usimamizi shirikishi wa kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe mkoani Tabora.

“Kada yetu ni kada maalumu kwa sababu inagusa maisha ya mwananchi moja kwa moja. Hivyo umaalumu huu usitufanye kuwa na viburi, bali utujengee moyo wa kuwahudumia wananchi wetu kwa uadilifu na moyo wa uzalendo,” amesema Prof. Nagu.



Aidha, amewataka watumishi wa sekta ya Afya kuwa na wivu wa kulinda taaluma yao kwa kuhakikisha wanazingatia maadili na miongozo iliyowekwa, pamoja na kuwaripoti watu wanaokiuka miiko ya kazi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Pia, Prof. Nagu ameelekeza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya za Halmashauri (CHMT) na Wahandisi wa Halmashauri katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Afya, ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia Sera, viwango na Miongozo ya Sekta ya Afya.



“usimamizi shirikishi na uwajibikaji wa pamoja kati ya wataalamu hao ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya Afya inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kuleta thamani halisi kwa wananchi, sambamba na kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.” amesisitiza Prof. Nagu.


No comments