Breaking News

WANANCHI WAASWA KUFUATA TARATIBU ZA KISHERIA WANAPOTAKA KUJENGA KUEPUKA USUMBUFU

 


Na Said Khamis.

Wananchi wametakiwa kufuata taratibu, kanuni na sheria za ujenzi ili kuipunguzia Serikali gharama zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) Mohammed Aboud Mohammed, wakati akizungumza na waandishi wa habari kando ya kikao cha bodi hiyo kilichofanyika katika Ofisi za ZBS, Amani Viwanda Vidogovidogo.

Mwenyekiti Mohammed alisema uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya wananchi hujenga bila idhini wala vibali rasmi vya Serikali, hali inayosababisha athari mbalimbali ikiwemo uharibifu wa ardhi na kuigharimu Serikali fedha nyingi kulipa fidia kwa wananchi waliovamia maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Alieleza kuwa kufuatwa kwa sheria na taratibu za ujenzi kutasaidia kuepusha migogoro ya ardhi na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Aidha, alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuleta maendeleo na kuboresha maisha ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.



Mwwnyekiti huyo alibainisha kuwa Bodi ya Wakurugenzi itaendelea kutoa ushauri kwa Serikali na kusimamia utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango bora, hususan katika ujenzi wa miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya nchi.

Aliongeza kuwa miradi hiyo inatoa fursa nyingi za ajira, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato cha wananchi kupitia harakati mbalimbali za maendeleo.

Mwenyekiti huyo alisema bodi itaendelea kusimamia maeneo yote ya ujenzi wa miradi mbalimbali ili kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa kuzingatia utaratibu, viwango vya kimataifa na ubora unaokidhi mahitaji ya wakati.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Majengo Zanzibar, Mhandisi Kassim Ali Omar, aliishauri Serikali kuwafanyia tathmini na upembuzi yakinifu baadhi ya wakandarasi na washauri elekezi wanaoshindwa kwenda sambamba na kasi ya utekelezaji wa miradi ya Serikali.


No comments