TAHADHARI ZA MAAMBUKIZI KWA VIJANA BADO ZINAHITAJIKA ILI KUMALIZA UKIMWI ZANZIBAR.
Na Siti Ali.
Licha ya serikali na wadau mbali
mbali kutoa elimu juu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa njia tofauti
lakini watu wengi hususani vijana wanapuuza tahadhari zinazotolewa na
kujiingiza katika tabia hatarishi zinazosababisha kupata maambukizi ya vvu na
ukimwi.
Ni vyema kila mtu aseme sasa basi
kila ajikinge na maambukizi ya ukimwi kwani njia moja wapo ya kupata usalama ni
kuepukana na tabia hatarishi,lakini sio vizuri kumdhania mtu kuwa
ameambukizwa,pia si vyema kumuamini mtu kuwa yupo salama kwa kumuangalia kwa
macho tu kwani macho kazi yake ni kuona.
Ifahamike kwamba kuona nje sura
ya mtu na umbo lake lakini ni vizuri kuwa na tabia ya kujichunguza mara kwa
mara ili kujua hali yako inavyoendelea hasa kwa kuangalia maambukizi ya vvu.
Inasikitika pia vijana wengi hujiingiza
katika vitendo vya kujamiiana katika umri mdogo ambapo baadhi yao wapo skuli za
msingi,sababu kuu ya zinazotajwa kwa vijana kujiingiza katika tabia hatarishi
zinazopelekea kuambukizwa virusi
vinavyosababisha ukimwi ni pamoja na mazingira ya kisasa yaliyotawaliwa na
utandawazi na kuwa mahodari wa kuiga maovu,kuwa na tamaa kushawishika na
teknolojia na kuendekeza shindikizo rika.
Watu waliomo kwenye kundi hili ni
wengi na wanaishi katika mazingira mchanganyiko miongoni mwao ni utashi,hamasa
hisia na mihemko ya kimaumbile ambayo hujiingiza katika ngono na hatimae hupata
vvu.
Kutokana na hali hii ipo haja ya
kutolewa elimu na nasaha ya mapema kwa vijana ili wasubiri, kwani kila kitu
kina wakati wake,imebainika kwamba kundi la vijana wenye umri wa miaka 9 hadi
24 ndio walio katika hatari Zaidi ya kuambukizwa vvu.
Jamii inatakiwa isisitize maadili
mema na mila nzuri za kizanzibar ili kuepuka kufanya ngono katika umri mdogo,kwani
watu watatu wa mwanzo wameambukizwa vvu hapa Zanzibar waligunduliwa mwaka 1986.
Tume ya ukimwi Zanzibar ZAC
wamekuwa mstari wa mbele katika kuongoza mapambano dhidi ya maambukizo mapya ya
vvu ili kutimiza lengo la kimataifa la kumaliza ukimwi ifikapo mwaka 2030.ZAC
imeendelea kutoa wito wa mashirikiano ya pamoja kwa wadau wote na kukumbuka
kwamba nguvu za pamoja katika kinga,tiba na huduma nyengine za ukimwi
zitatufikisha kwenye lengo lililokusudiwa la kumaliza ukimwi duniani.
Akieleza hali ya maambukizi ya
ukimwi Zanzibar Mwenyekiti wa bodi ya Tume ya UKIMWI Zanzibar Dr Ali Salim Ali
amesema kuwa kwa mwaka wa 2025kupitia vituo vinavyotoa huduma za ushauri nasaha
na uchunguzi wav vu,jumla ya watu 105,756walipimwa kati yao wanawake walikuwa
58,359 sawa na asilimia (55%)na wanaume ni 47,397sawa na asilimia (45%).
“Katika takwimu hizi watu 79,526
sawa na asilimia (75%)walipimwa Unguja na 26,230(25%)walipimwa Pemba .Jumla ya
watu 697sawa na asilimia 0.7)waligundulika na maambukizi ya vvu ,kati ya hao
wanawake ni 466 sawa na asilimia (67%)na wanaume ni 231 sawa na asilimia (33%)”ameeleza
Dr Salim.
Aidha ameendelea kusema kuwa
takwimu za maambukizi ya kwa umri zinaonesha kuwa kundi lenye maambukizo mengi
Zaidi ni la umri wa miaka 25-49 ambalo linachangia asilimia 71% ya maambukizo
yote yaliyorikodiwa likifuatiwa na kundi la umri wa miaka 20-24.Takwimu hizi
zinaashiria uhitaji wa kuimarisha mikakati ya kinga na elimu ya vvu,pamoja na
kuendelea kuelimisha vijana ili kupunguza tabia hatarishi walizonazo.
Sambamba na hayo amesema juhudi
za kuzuia maambukizo ya vvu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zimeonesha
mafanikio makubwa.Hadi kufikia septemba jumla ya wajawazito 53,706 walihudhuria
klinik kati yao kinamama 53,031 walifanyiwa vipimo vya vvu,ikiwa ni sawa na
asiimia 99%ya waliohudhuria kliniki.
“Miongoni mwa kinamama waliopimwa
89 walikutwa na maambukizi ya vvu ambao ni sawa na asilimia 0.2 ya wale
waliopimwa.Kwa watoto waliozaliwa na mama wenye vvu ,jumla ya watoto 362
walipimwa kwa kutumia kipimo cha DNA-PCR,kati yao watoto wawili 2 waligundulika
na vvu ambao ni sawa na asilimia 0.5% ya kiwango cha maambukizo.Mafanikio haya
yanaonesha maendeleo chanya katika kufikia hatua ya kumaliza maambukizo ya vvu
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”ameeleza Dr Ali.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya
ukimwi duniani huko katika ukumbi wa sheikh Idrisa Abdulwakil kikwajuni makamo
wa pili wa Zanzibar Mh Hemed Sueiman Abdulla amesema kuwa Zanzibar imefanikiwa
kupunguza maambukizi mapya ya maradhi ya ukimwi kutoka watu 362 kwa mwaka 2020
hadi kufikia watu 211 waliopata maambukizi mapya ya kwa mwaka 2025 jambo
lililosaidia kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi ya ukimwi kutoka vifo 230
kwa mwaka 2020 hadi vifo 115kwa mwaka 2025.
Mh Hemed amefahamisha kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa mpango maalumu unaojulikana kwa jina
la “Mpango endelevu wa kupambana na Ukimwi Zanzibar”wenye lengo la la kuhakikisha
mapambano dhidi ya ukimwi yanakuwa endelevu ili kufikia lengo la kumaliza
ukimwi ifikapo 2030.
Aidha Makamo wa pili wa rais
amewahakikishia watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kuwa serikali inayoongozwa
na Dkt.Hussein Mwinyi itazifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na jumuiya
ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi Zanzibar (ZAPHA+) ikiwemo kuongezwa
bajeti kwa ajili ya upatikanaji wa dawa na vipimo kwa wagonjwa wa ukimwi,pia
kuwezesha harakati za mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi nchini.
“Nawasihi wananchi
kutowanyanyapaa na kuwabagua watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kwani kufanya
hivyo ni kurudisha nyuma jitihada za serikali za kumaliza maambukizi mapya ya
ukimwi”amesema Mh Hemed.
Hata hivyo ametoa wito kwa
taasisi wadau na jamii kwa ujumla kushirikiana na kwa pamoja katika kuhamasisha
kampeni za mabadiliko ya tabia ,kuongeza ubunifu na upatikanaji wa fedha na
vifaa ambavyo vikitumika kwa ufanisi lengo la kumaliza ukimwi Zanzibar
litafikiwa.
“Natoa wito kwa taasisi wadau na
jamii kwa ujumla kushirikiana na kwa pamoja katika kuhamasisha kampeni za
mabadiliko ya tabia ,kuongeza ubunifu na upatikanaji wa fedha na vifaa ambavyo
vikitumika kwa ufanisi lengo la kumaliza ukimwi Zanzibar litafikiwa ameeleza Mh
Makamo.
Nao watu wanaoishi na virusi vya
ukimwi Zanzibar kutoka jumuiya yya ZAPHA+ wamesema kuwa kutokana na mashirika
na wafadhili kusuasua katika kutoa misaada hasa kwa watu wanaoishi na virusi
vya ukimwi wameiombaserikali kuliangalia suala la dawa za ARV kuwekwa katika
bajeti ya serikali ili huduma hiyo iendelee kwa wagonjwa wa ukimwi.
“Tunakabilwa na changamoto mbali
mbali hii inatokana na mashirika na wafadhili kusuasua katika kutoa misaada
hasa kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi hivyo basi tunaiomba serikali
kuliangalia suala la dawa za ARV na kuweka katika bajeti ya serikali ili huduma
hiyo iendelee kwa wagonjwa wa ukimwi”wameeleza watu hao.
Aidha wamesema kuwa wagonjwa wa
ukimwi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto katika sehemu za utoaji wa huduma za
kijamii hivyo wameiomba serikali kuwasaidiwa kutambulika kupitia katika mifumo
mbali mbali ya utoaji wa huduma hasa hospitali ili waweze kupatiwa huduma ambazo
zitapelekea kuwaondoshea usumbufu.
“Tunaiomba serikali kutusaidia
kutambulika katika mifumo mbali mbali ya utoaji wa huduma hasa hospitali ili tuweze
kupatiwa huduma ambazo zitapelekea kutuondoshea usumbufu”wamesema.
Sambamba na hayo wamesema kuwa
katika kukabiliana na usumbufu dhidi ya ukimwi,hivyo basi serikali inapaswa
kuanzisha mfumo maalumu mapambano dhidi ya ukimwi ambao utakabiliana na
upungufu wa fedha kwa ajili ya upatikanaji wa huduma muhimu kwa watu wanaoishi
na ugonjwa wa ukimwi
Vile vile usiwaamini moja kwa
moja wanaodai kuwa wamepimwa na kuonekana salama kwa kuwa ana cheti kwani kuwa
na cheti sio usalama wa kudumu,inawezekana alopimwa jana au mwezi uliopita leo
akagundulika na VVU,hivyo basi kila mmoja wetu anapaswa kuwa makini kwa kuwamua
kwa makusudi kupima afya yake na kuachana na tabia zinazohatarisha maisha.
Jamii inatakiwa kuchukuwa
tahadhari kubwa kwa ugonjwa huu ambao athari zake zinasikitisha sana kwa kuwepo
unyanyapaa na kuongezeka watoto wanaoishikatika mazingira magumu kwani muda
mrefu tumeshuhudia ndugu zetu wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huu,na tunaweza
kusema kwamba hakuna familia ambayo haijaguswa na ugonjwa huu.
Hivyo basi kila mmoja achukuwe
tahadhari juu ya ugonjwa huu kwani kinga
ni bora kuliko tiba.


No comments