Breaking News

JESHI LA POLISI LAHAKIKISHA USALAMA WA WANANCHI KIPINDI CHA SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA ZANZIBAR



Na said Khamis.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja limewahakikishia wananchi kuendelea kudumisha usalama na amani katika kipindi cha Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya, huku likisisitiza kuwa halitaruhusu mtu au kikundi chochote kutumia sikukuu hizo kufanya vitendo vya kihalifu.

Akizungumza kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, Jeshi la Polisi limesema kuwa limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo kabla, wakati na baada ya sikukuu hizo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja linapenda kuwahakikishia wananchi kwamba litaendelea kudumisha usalama na amani katika kipindi hiki cha Sikukuu za Mwisho wa Mwaka, hivyo hakutakuwa na nafasi ya mtu au kikundi cha watu kutumia sikukuu hizo kama sehemu ya kufanya uhalifu,” imesema taarifa hiyo.

Jeshi la Polisi limetaja kuwa kila ifikapo tarehe 25 Disemba, Wakristo Zanzibar huungana na waumini wenzao duniani kote kusherehekea Sikukuu ya Krismas, ambayo huambatana na ibada, mkesha pamoja na shamrashamra mbalimbali, huku tarehe 26 Disemba ikiwa ni siku ya Boxing Day. Aidha, tarehe 01 Januari huadhimishwa kama Sikukuu ya Mwaka Mpya.

Katika kipindi hicho, Jeshi la Polisi limewataka madereva wa vyombo vya moto, ikiwemo magari na pikipiki, pamoja na watumiaji wengine wa barabara, kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

“Hakutakuwa na muhali wala huruma kwa madereva wanaotumia magari kufanya misère (drifting), kwani vitendo hivyo vinasababisha uharibifu wa miundombinu na kuhatarisha maisha ya watumiaji wengine wa barabara,” imesisitiza taarifa hiyo.

Jeshi la Polisi pia limewakumbusha wazazi na walezi kuchukua tahadhari zaidi kwa watoto wao, hasa kipindi hiki ambacho shule zimefungwa na watoto hutumia muda mwingi katika maeneo ya starehe.

“Tunawaomba wazazi na walezi kutowaachia watoto wadogo kwenda peke yao katika viwanja vya starehe, kwani katika kipindi cha sikukuu kumekuwa na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia na udhalilishaji wa watoto,” imeeleza taarifa hiyo.


 

Kwa upande mwingine, wamiliki wa kumbi za starehe wametakiwa kuendelea kufuata sheria na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa vibali vyao. Jeshi la Polisi pia limewataka wananchi kuzingatia muda unaoruhusiwa wa kutumia fukwe, ambapo matumizi ya fukwe yatakoma saa 12:00 kamili jioni.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja limeonya kuwa halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayekiuka sheria, ikiwemo kumfikisha mahakamani.


No comments