Breaking News

MAMLAKA ZA MAPATO AFRIKA MASHARIKI KUJA NA MBINU MPYA DHIDI YA UHALIFU NA RUSHWA.

 


Na Said Khamis.

MAMLAKA za Mapato Afrika Mashariki zimesisitizwa kuimarisha matumizi ya ushahidi wa kitaalamu (forensic evidence) katika mapambano dhidi ya rushwa na uhalifu wa kifedha ili kulinda mifumo ya mapato na kuimarisha uadilifu wa taasisi za umma.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Said Kiondo Athumani, wakati akifungua mkutano wa 21 wa Kamati ya Kiufundi ya Uadilifu ya Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki uliofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni.

Alisema kuimarisha uadilifu ni msingi muhimu wa kuboresha ukusanyaji wa mapato, kulinda uhalali na kuimarisha taswira ya mamlaka za mapato pamoja na nchi kwa ujumla, hasa katika kipindi ambacho nchi za ukanda zinaelekea zaidi katika ujumuishaji wa kiuchumi.

Kamishna Kiondo alieleza kuwa wahalifu wa kifedha na wakwepaji kodi hubuni mbinu mpya kila siku, hali inayohitaji mamlaka za mapato kutumia teknolojia na ushahidi wa kisasa wa kitaalamu ili kukabiliana na uhalifu huo unaovuka mipaka ya kijiografia.

Alibainisha kuwa rushwa katika mamlaka moja huathiri ukanda mzima, kwani mitandao ya kihalifu hutumia mianya iliyopo katika taasisi zilizo dhaifu, hivyo kufanya ushirikiano wa kikanda na ubadilishanaji wa taarifa kuwa jambo la lazima.

Akizungumzia kaulimbiu ya mkutano huo isemayo “Kuimarisha Mapambano Dhidi ya Rushwa Kupitia Ushahidi wa Kitaalamu (Forensic Evidence)”, alisema inalenga kuongeza usahihi wa uchunguzi, kupunguza uingiliaji wa ndani na kuongeza imani ya umma kwa mamlaka za mapato.

Aliwahimiza wajumbe wa mkutano huo kushiriki kwa uwazi, kubadilishana uzoefu, kujadili kesi halisi na kuimarisha matumizi ya teknolojia ya forensics pamoja na kujenga uwezo wa ndani wa uchunguzi katika mamlaka zao.



Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Abola, alisema nchi wanachama zimekubaliana kuimarisha hatua za kinga, uchambuzi wa hatari za uadilifu na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma.


No comments