ZAGCO YAIBUKA NA MBEGU MPYA YA MAHINDI MATAMU ZANZIBAR.
NA SALAMA MOHAMMED, WKUMM
NAIBU Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk. Salum Soud Hamed, ameipongeza taasisi ya Zanzibar Green Culture Organisation (ZAGCO) na kampuni ya East West Seed kwa kushirikiana na Wizara hiyo na kufanikisha majaribio ya mbegu mpya ya mahindi matamu hatua iliyowajengea vijana uelewa na umahiri wa matumizi sahihi ya pembejeo pamoja na teknolojia za kisasa.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya ‘Shamba Darasa’ yaliyowakutanisha vijana wanaohitimu na wanaoendelea na masomo ya kilimo na mifugo, katika viwanja vya maonesho Dole Kizimbani, wilaya ya Magharibi 'A', Dk. Salum alisema mafunzo hayo ni kielelezo cha uzalendo na vitendo vinavyolenga kuandaa kizazi cha wataalamu wabunifu.
Alisema vijana wana nafasi kubwa ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kukifanya kuwa chanzo kikuu cha ajira, kipato na maendeleo ya taifa.
“Nimefarijika kusikia kuwa ZAGCO inaunganisha vijana wahitimu na wanaoendelea na masomo ya kilimo ili kuwaongezea ujuzi wa vitendo. Huu ni msingi muhimu wa kujenga kilimo chetu cha kisasa”, alisema Dk. Salum.
Alieleza kuwa kilimo hakiwezi kutegemea vitabu pekee bali kinahitaji mafunzo ya moja kwa moja shambani na akaitaka ZAGCO kuendeleza jitihada hizo sambamba na malengo ya serikali ya awamu ya nane kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha Dk. Salum alibainisha kuwa ZAGCO ni taasisi inayoundwa na vijana waliobobea katika masomo ya kilimo kutoka vyuo mbali mbali, hatua ambayo imeonesha mabadiliko yanayolengwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kupitia mageuzi ya kilimo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zan
zibar (ZALIRI), Dk. Abdalla Ibrahim Ali, aliipongeza ZAGCO kwa hatua ya kuwaunganisha vijana na wakulima kupitia mafunzo hayo, akisema ushirikiano wa pamoja ni nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya kilimo.
Alisema taasisi hiyo ina malengo makubwa ya kufanya tafiti za kisasa katika kilimo na mifugo, hivyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa vijana hao ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi ili kuboresha mafunzo ya vitendo.
Akisoma risala ya jumuiya hiyo, Mkurugenzi wa ZAGCO, Hussein Ame Vuai, alisema jumuiya hiyo inaundwa na vijana waliomaliza au wanaoendelea na masomo ya kilimo, mifugo na uvuvi katika ngazi mbali mbali kutoka Skuli ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SOA – SUZA) na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA).
Alisema lengo la jumuiya hiyo ni kuwaongezea vijana ujuzi, kuwawezesha kupata fursa za ajira pamoja na kuanzisha miradi yenye tija nakubainisha changamoto ya uhaba wa miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo ya shamba darasa na kuiomba serikali kusaidia kutatua changamoto hizo.
Mafunzo hayo yalishirikisha wataalamu kutoka Kampuni ya East West Seed, maafisa kilimo wa wilaya, wakulima pamoja na wanafunzi wa fani za kilimo, ambapo jumla ya wanachama 52 walihudhuria wakiwemo wanawake 29 na wanaume 23.
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
No comments