Udhalilishaji wa Kijinsia haupaswi Kuvumiliwa Taasisi ya Elimu ya Juu Dkt Mkuya.
Na Abdul Sakaza.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Saada Mkuya Salum, amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu Zanzibar kulinda maadili, kuheshimu utu wa wengine na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia, an kuisisitiza kuwa udhalilishaji haupaswi kuvumiliwa katika taasisi za elimu ya juu.
Dkt. Mkuya alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wapya wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, wakati wa Wiki ya Ukaribisho wa Wanafunzi, Mkutano huo ulilenga kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa madawati ya jinsia na namna ya kuyatumia kupata msaada wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali.
Alisema kujiunga na chuo kikuu ni fursa muhimu ambayo wanafunzi wanapaswa kuitumia kwa kuzingatia malengo yao ya kitaaluma, nidhamu na uwajibikaji, akibainisha kuwa si kila mwenye ndoto ya kupata elimu ya juu anayefanikiwa kupata nafasi hiyo.
Alieleza kuwa wanafunzi wanapaswa kujenga msingi imara wa maisha yao ya baadaye kwa kufanya maamuzi sahihi, kujituma katika masomo na kuepuka vitendo vinavyoweza kuwakwaza katika safari yao ya kielimu.
Aidha, aliwahimiza kujitambua, kuheshimu mipaka yao na kuchagua marafiki wanaoweza kuwasaidia kufikia malengo yao, akionya kuwa starehe zisizo na mipaka zinaweza kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma.
Hata hivyo Dkt. Mkuya aliwataka wanafunzi kuepuka mahusiano yasiyofaa na walimu kwa lengo la kupata alama za juu, akisisitiza kuwa mafanikio ya masomo yanapaswa kutokana na juhudi, uwezo na uadilifu wa mwanafunzi. Pia aliwataka kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na kuielekeza katika shughuli za kujifunza na kujijengea maarifa.
Akizungumzia suala la ukatili wa kijinsia, alisema wanafunzi hawapaswi kukaa kimya wanapofanyiwa vitendo vya udhalilishaji au kushuhudia wengine wakikumbwa na matukio hayo. Aliwahimiza kutoa taarifa kupitia madawati ya jinsia, mamlaka husika au Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Aliongeza kuwa madawati hayo yana umuhimu mkubwa katika kutoa elimu, ushauri nasaha na msaada kwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto za afya ya akili na matatizo mengine yanayoweza kuathiri ustawi wao.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Abdi Talib Abdalla, aliwapongeza wanafunzi wapya waliochaguliwa kujiunga na chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2026/2027, akiwataka kutumia nafasi hiyo kwa bidii, nidhamu na uwajibikaji.
Prof. Abdi aliwahimiza wanafunzi kujenga utamaduni wa kushirikiana, kuunda mitandao mizuri ya kitaaluma na kufanya kazi kwa pamoja, akieleza kuwa ushirikiano ni muhimu katika kuboresha maendeleo ya masomo yao na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha baada ya kuhitimu.
Pia aliwataka kuzingatia malengo yaliyowapeleka chuoni, kuepuka unyanyasaji wa aina yoyote na kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima inayoweza kuvuruga masomo yao.
Akifafanua juhudi za chuo katika kupambana na ukatili wa kijinsia, Prof. Abdi alisema SUZA ina Dawati la Jinsia ambalo limekuwa likifanya kazi tangu mwaka 2023, likiongozwa na sera inayobainisha majukumu yake na namna ya kutekeleza shughuli zake.
Alisema chuo kina mkakati wa kuliboresha dawati hilo na kulifanya kuwa kituo maalumu kitakachosaidia kuimarisha utoaji wa elimu, ushauri na huduma za msaada kwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali.
Vilevile, aliwakumbusha wanajumuiya ya SUZA kuwa chuo hicho kinatimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake mwaka huu, ambapo shughuli mbalimbali za kijamii na kitaaluma zimepangwa kuadhimisha hatua hiyo muhimu katika historia ya taasisi hiyo.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah, aliwapongeza wanafunzi wapya kwa kuanza safari ya elimu ya juu, huku akiwataka kuwa makini na changamoto zinazoweza kujitokeza katika mazingira mapya ya maisha ya chuoni, ikiwemo ukatili wa kijinsia.
SACP Shillah alisema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na madawati ya jinsia pamoja na taasisi nyingine katika kutoa elimu kwa umma na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aliwasisitiza wanafunzi kuzingatia maadili mema, kuepuka mazingira hatarishi na kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapobaini matukio ya ukatili, ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa.
Hafla hiyo iliwashirikisha wanafunzi kutoka SUZA na taasisi nyingine za elimu ya juu Zanzibar, zikiwemo KIST, Zanzibar School of Health, SUMAIT University, Open University of Tanzania, Zanzibar University, Zanzibar School of Law na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Zanzibar.
Utoaji wa elimu kuhusu madawati ya jinsia ni sehemu ya juhudi za SUZA za kuhakikisha wanafunzi wanafahamu haki zao na mifumo iliyopo ya kupata msaada, kwa lengo la kujenga mazingira salama ya kujifunzia yanayozingatia heshima, usawa na ustawi wa kila mwanafunzi.




No comments