TAMWA Zanzibar Yazifikia Shule Kuimarisha Ulinzi wa Mtoto wa Kike
Mtoto wa kike
ana haki ya kuishi katika mazingira salama, kupata elimu, kushiriki katika
nafasi za uongozi na kulindwa dhidi ya aina zote za udhalilishaji, ikiwemo
ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni. Hata hivyo, utekelezaji wa haki hizo
unahitaji ushirikiano wa familia, skuli, jamii na taasisi zinazohusika na
ustawi na ulinzi wa watoto.
Katika
kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA Zanzibar) kimepeleka elimu kwa wanafunzi wa
Skuli ya Msingi Kinyasini, Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, na Skuli ya Msingi
Dunga pamoja na Bambi, Mkoa wa Kusini Unguja, kwa lengo la kuwajengea uelewa
kuhusu haki zao, namna ya kujikinga na udhalilishaji pamoja na umuhimu wa
kujitambua na kujiamini.
Akizungumza
kuhusu umuhimu wa kulinda haki za watoto wa kike, Bi. Safia Ngalapi, Meneja wa
Mawasiliano wa chama hicho , amesema mtoto wa kike ana haki ya kulindwa dhidi
ya aina zote za udhalilishaji na kupatiwa haki zake zote.
Ngalapi
ameongeza kuwa utoaji wa elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha watoto,
walimu na jamii kwa ujumla kutambua kuwa ulinzi wa mtoto wa kike si jukumu la
familia pekee, bali ni wajibu unaohusisha skuli, jamii, taasisi za serikali na
mashirika yanayotetea haki za watoto.
Akitoa elimu kwa
wanafunzi wa Skuli ya Msingi Kinyasini, Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya
Kaskazini A, Makame Makame, ameeleza umuhimu wa Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa
Kike katika kuhamasisha jamii kutambua haki, mahitaji na changamoto
zinazowakabili watoto wa kike.
Amesisitiza
umuhimu wa kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa sawa za kukua, kujifunza
na kufikia malengo yao bila kukabiliwa na vitendo vinavyoweza kuhatarisha
usalama wao au kuathiri mustakabali wa maisha yao.
KWANINI TAMWA
ZANZIBAR IMEPELEKA ELIMU MASHULENI?
Akizungumzia
maadhimisho hayo, Hairat Haji, Afisa Programu kutoka TAMWA Zanzibar, amesema
Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike huadhimishwa ili kukumbusha jamii wajibu
wake katika kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa
kijinsia na kuhakikisha wanapata haki zao.
Amesema TAMWA
Zanzibar imeamua kupeleka elimu hiyo mashuleni ili kupata fursa ya kuzungumza
moja kwa moja na wanafunzi kuhusu changamoto zinazoweza kuathiri maisha yao na
namna wanavyoweza kutafuta msaada wanapokabiliwa na vitendo vya ukatili.
“Shule ni
miongoni mwa maeneo muhimu katika kuimarisha ulinzi wa watoto kwa sababu walimu
na walezi wanaweza kusaidia kutambua mabadiliko katika mwenendo wa mwanafunzi,
kutoa muongozo na kuwaunganisha watoto wanaohitaji msaada na mamlaka husika,”
amesema Khairat.
Ameeleza kuwa
elimu kuhusu haki za mtoto wa kike inapaswa kuendelea kutolewa ili kuwasaidia
wanafunzi kutambua vitendo vya udhalilishaji, kuelewa haki zao na kujua mahali
pa kuripoti wanapokabiliwa na changamoto zinazohatarisha usalama wao.
Katika hatua
nyingine, Khairat amewataka watoto wa kike kujitambua na kuthubutu kugombea
nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kujiamini na
kutumia fursa zinazopatikana shuleni na katika jamii.
WAZAZI NA
JAMII WATAKIWA KUUNGA MKONO JUHUDI HIZO
Kwa upande wake,
Adam Haruna, mchambuzi wa masuala ya elimu na jinsia, amesema juhudi za TAMWA
Zanzibar zinahitaji kuungwa mkono na wazazi na walezi kwa kuwajengea watoto
mazingira ya kuzungumza kwa uhuru kuhusu changamoto wanazokutana nazo, bila
hofu ya kulaumiwa, kutishwa au kudhalilishwa zaidi.
“Mtoto anapopata
nafasi ya kueleza tatizo lake na kusikilizwa, inakuwa rahisi zaidi kwa watu
wanaowajibika kuchukua hatua zinazofaa kumlinda na kumsaidia,” amesema Adam
Haruna.
Amesisitiza
umuhimu wa jamii kushirikiana katika kuhakikisha watoto wa kike wanakua katika
mazingira yanayowapa nafasi ya kupata elimu, kujenga uwezo wao na kutimiza
ndoto zao.
UJUMUISHI NI HAKI
Mafunzo hayo
hayakuacha nyuma masuala ya ujumuishi wa jinsia zote katika kupata elimu,
nafasi za uongozi na haki ya kushiriki na kushirikishwa. Mbaya Ali Haji kutoka
baraza la watu wenye ulemavu ameelezea watoto wenye ulemavu wana haki ya
kupendwa kusaidiwa , kusikilizwa fikra na mitazamo yao pia kupewa fursa sawa
bila kujali haliya ulemavu wao.
‘’Ni makossa kisheria
kumuita majina mabaya mtu mwenye ulemavu , hapa nitayataja majina ambayo ni
sahihi kuwaita watu wenye ulemavu, kuna kiziwi, mtu mwenye ulemavu wa viungo,
asieona, na mtu mwenye ualbino’’
Akizungumzia Atari
za ndoa za umri mdogo Afisa Programu wa TAMWA-ZNZ Asia Hakim ameeleza kuwa
watoto wa kike hushindwa kufikia malengo yao baada ya kuolewa katika umri mdogo
jambo ambalo huwafanya washuke kiuchumi, hukosa fursa za kujishuhulisha na
uongozi, na badala yake kubaki kuwa tegemezi katika maisha yao.
HISTORIA SIKU YA MTOTO WA KIKE
Kwa mujibu wa
Umoja wa Mataifa, Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ilitangazwa rasmi na
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 19 Desemba 2011 kupitia Azimio namba
66/170, na maadhimisho ya kwanza yalifanyika tarehe 11 Oktoba 2012.
Tangu wakati
huo, siku hiyo imekuwa fursa ya kimataifa ya kuhamasisha serikali, mashirika ya
kiraia, familia na jamii kuimarisha hatua za kulinda haki za watoto wa kike na
kuhakikisha wanapata fursa za kuendeleza vipaji na uwezo wao.
Maadhimisho hayo
yanaangazia changamoto zinazowakabili watoto wa kike, zikiwemo ukatili wa
kijinsia, ndoa za utotoni, ubaguzi na vikwazo vinavyoweza kuwanyima fursa ya
kupata elimu na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii ambapo Kaulimbiu
ya mwaka 2026 ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ni “Komesha ndoa za
utotoni na wekeza katika haki za mtoto wa kike.”
Kaulimbiu hiyo
inasisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja kuzuia ndoa za utotoni na
kuwekeza katika elimu, ulinzi na maendeleo ya watoto wa kike huku Juhudi za
TAMWA Zanzibar za kutembelea skuli na kutoa elimu zinaongeza nafasi ya
kuwafikia wanafunzi moja kwa moja.
.jpeg)

.jpeg)


No comments