Breaking News

Mtoto Aliyeripotiwa Kupotea Apatikana Amefariki Eneo la Mikoko Wilayani Mkoani, Pemba

NA JUMA SEIF.

Mtoto Mnabi Ali Kombo mwenye umri wa miaka 12 amefariki dunia katika eneo lenye mikoko,Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, baada ya kuripotiwa kupotea siku ya Jumanne.  Taarifa za awali zinahusisha tukio hilo na mgogoro wa kifamilia kuhusu malezi ya watoto.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, mtoto huyo aliripotiwa kwa Sheha kuwa amepotea siku ya Jumanne. Wakati huo, wazazi wake walikuwa katika mgogoro wa kifamilia kuhusu malezi ya watoto, suala ambalo lilikuwa tayari limefikishwa katika Mahakama ya Kadhi kwa ajili ya kushughulikia madai yanayohusu watoto na talaka.

Inadaiwa kuwa wazazi hao, licha ya kutokuwa wametengana rasmi, walikuwa wakiishi maeneo tofauti ndani ya mji huo huo. Siku ya Jumanne, baba wa watoto alifika kutoka Unguja kwenda kwa mama wa watoto, akidaiwa kuwa na lengo la kufuatilia suala la watoto.

Kutokana na hali hiyo, kila mzazi alikuwa na mashaka kuhusu alipo mtoto huyo. Mama alihisi huenda baba alimchukua mtoto bila taarifa zake, huku baba naye akihisi huenda mama alikuwa amemficha mtoto.

Siku iliyofuata, Jumatano, wazazi hao walielekezwa kufika Mahakama ya Kadhi wakiwa na watoto wote, kila mmoja akiamini kuwa mwenzake angekuwa amemleta mtoto aliyepotea. Hata hivyo, walipofika mahakamani, ilibainika kuwa mama alikuwa na mtoto mmoja, huku baba akiwa hana mtoto huyo aliyekuwa akitafutwa.

Katika maelezo yaliyotolewa wakati wa kujaribu kufahamu alipo mtoto huyo, mama alieleza kuwa alifahamishwa kwamba mtoto alikuwa ameondoka asubuhi. Alidai kuwa hakumfuata mtoto huyo, kwa kuwa hakuwa naye, na aliporudi kumtafuta hakumkuta. Hali hiyo ilimfanya ahisi huenda baba wa mtoto alimchukua.




No comments