WIZARA YA UJENZI, TAWALA ZA MIKOA NA MANISPAA MJINI, YAPEWA WIKI MOJA KUISHUGHULIKIA MITARO INAYOTUWAMA MAJI TAKA.
NA SITI ALI.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema haridhishwi na hali ya uchafu uliokithiri katika Mitaro yakupitishia maji taka iliyopo katika maeneo mengi ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua Mitaro yakupitishia maji taka iliyopo katika maeneo ya Mfenesi Mazizi, Mayugwani kwa wagonga vyuma hadi TRA , Gulioni mbele ya Ofisi ya zamani ya Mamlqka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Makao Makuu ya Shirika la Umeme zanzibar ( ZECO ).
Amesema hali ya usafi hairidhishi katika maeneo yote aliyotembelea kutokana na kukosekana kwa mipango madhubuti ya kufanyika usafi endelelvu katika mitaro hio ambayo inahatarisha afya za wakaazi wa maeneo hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametoa wiki moja kwa Wizara ya ujenzi na uchukuzi kwa kushirikiana na taasisi nyengine kuhakikisha maeneo yote yenye mitaro ambayo maji hayatembei inavyotakiwa inafanyiwa matengenezo ili kuweka mazingira safi na kulinda afya za wananchi katika kipindi hichi cha kuelekea mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha zikiambatana na mvua za ELNINO.
Amesema katika kupambana na kudhibiti hali ya uchafu katika maeneo mbali mbali ya Mji wa Zanzibar viongozi wanapaswa kushuka kwa wananchi kuwapatia elimu juu ya athari zinazotokana na kuishi katika mazingira machafu yanayoweza kusababisha maradhi ya mripuko ambayo yanaweza kudhibitiwa kwa kujenga tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao wanayoishi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametoa agizo kwa Baraza la Manispaa Mjini kuhakisha usafi unafanyika katika maeno yote ya Mjini na unakuwa endelevu hasa katika maeneo yenye changamoto kubwa ya uchafu na kusema kuwa haipendezi kufanyika usafi kutokana na kuwepo kwa tahadhari ya mvua za ELNINO bali suala la usafi liwekwe katika ratiba zao za kazi za kila siku za kuhakisha mji unakuwa safi.
Sambamba na hayo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi na wafanya biashara katika maeneo ya Mayugwani kwa wagonga vyuma kuendelea kuwa wastahmilivu wakati Serikali ikiendelea kulipatia ufumbuzi suala la kufanyiwa usafi Mtaro wa kupitishia maji machafu uliopo katika eneo hilo pamoja na kuwaomba kuridhia kuondoka katika eneo hilo ili kupisha mipango ya Serikali iendelee.
Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ ndugu ISSA MAHFOUDH HAJI amesema Wizaraya yake kwa kushirikiana na Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar na Taasisi nyengine tayari wameanza operesheni ya kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Mjini ambapo Operesheni hio itakuwa endelevu kwa maenneo yote hasa yale hatarishi yaliyomo ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katibu Mkuu ISSA amesema Mitaro ambayo imekuwa ikituwama maji machafu kwa muda mrefu imetokana na ujenzi wa miundombinu ya barabara inayoendelea kujengwa ndani ya Mkoa wa Mjini Magharabi ambapo hatua za kuitatua changamoto hio zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wanaondokana na kero hio na kuendelea kuishi katika mazingira safi na salama.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya wa Mjini Dkt. SAID HAJI MRISHO amesema Serikali ya Wilaya imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali katika kuhakikisha mitaro hio inakuwa safi na salama na kusema kwamba nguvu za pamoja zinahitajika katika kuhakikisha mitaro hio inafanyiwa matengenezo makubwa ili iweze kuruhusu maji kupita bila ya kikwazo cha aina yoyote.
Katika ziara hio Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar ametembelea Maeneo ya MFENESI MAZIZI – Gulioni, MAUGWANI KWA WAGONGA VYUMA – TRA ,Gulioni, Ofisi ya zamani ya ZAWA, pamoja na eneo la GULIONI MBELE YA MAKAO MAKUU YA ZECO.


No comments