.MFUMO WA ZCP, DARAJA BAINA YA SMZ NA WAFANYABIASHARA.
NA SITI ALI.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuboresha miundombinu ya usafirishaji, matumizi ya TEHAMA, nishati ya umeme na kuweka sera zinazoziwezesha sekta binafsi kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa Jumuia ya Kitaifa ya wafanyabiasha Zanzibar ( ZPC ) uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema majadiliano ya pamoja kati ya Serikali na Sekta binafsi pamoja na uzinduzi wa mfumo wa Jumuia ya Kitaifa ya wafanyabiasha Zanzibar utaleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma na ukuzaji wa sekta binafsi kupitia teknolojia ya kisasa inayokwenda kwa kasi duniani kote.
Mhe. Hemed amesema azma ya Serikali kwa sekta binafsi ni kuhakikisha zinatumia teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ushindani wa kibiashara katika soko la Kikanda na Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya Teknolojia Duniani, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kufanya mageuzi makubwa ya teknolojia katika kuweka Sera, usimamizi wa uchumi na uboreshaji wa mazingira ya sekta binafsi ikiwemo sekta ya biashara ili kuweza kuvutia wawekezaji na kushindana katika uchumi wa dunia.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais amefahamisha kuwa kupitia Mfumo wa Zanzibar Chamber Potal ( ZCP ) utaweza kuwasaidia wanajumuia ya Kitaifa ya Wafanyabiasha wa Zanzibar kuweza kupata huduma nyingi kwa urahisi ikiwa ni pamoja na usajili na uhuishaji wa wanachama, maombi ya vyeti vya uasili wa bidhaa, uwasilishaji wa changamoto za biashara na vikwazo visivyo vya kodi pamoja na kufatilia maendeleo ya maombi yao kupitia mfumo huo.
Sambamba na hayo, Mhe. Hemed amesema mfumo huo utakuwa ni daraja la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi katika nukussnyaji wa taarifa zilizo sahihi na kwa wakati ambazo zitaiwezesha Serikali kutambua kwa urahisi changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kufanya maamuzi katika kuboresha Sekta ya biashara.
Hata hivyo Mhe. Hemed amezihimiza taasisi zote za Serikali kuiona Kamati ya Kitaifa ya kushughulikia vikwazo visivyo vya kodi kama mshirika wa kuboresha huduma na sio mkosoaji wa utendaji wao wa kazi pamoja na kuwahimiza wafanyabiasha kutumia njia rasmi ya kuwasilisha changamoto zao kupitia mfumo wa ZPC na kamati husika.
Nae Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Umbunifu Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka msingi imara wa mageuzi ya kidijitali kupitia uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya TEHAMA, huduma za kidijitali na mifumo ya kisasa ya utoaji huduma kwa njia ya kiteknolojia ambayo imekuwa nyenzo ya kuongeza tija katika sekta biashara, utalii, afya, elimu, kilimo, uvuvi hadi utoaji wa huduma za Serikali.
Mhe. Soraga amesema azma ya Serikali ni kufikia hatua ambayo mifumo ya Serikali na taasisi mbali mbali itaweza kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa usalama na ufanisi ( INTEROPERABILITY ), ili wananchi na wafanyabiashara wasihitajike kutoa taarifa zilezile na mara kwa mara wanapotafuta huduma.
Aidha, Mhe. SORAGA ameweka msisitizo kwa Jumuia ya Kitaifa ya wafanyabiasha wa Zanzibar kuanza kujiandaa kwa hatua ya uchumi wa kidijitali kwa kuwekeza katika matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence), uchambuzi wa taarifa (data analytics) na ubunifu wa kidijitali ili kufanya maamuzi bora zaidi, kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha ushindani wa Zanzibar katika uchumi wa dunia unaobadilika kwa kasi.
Mapema Mwenyekiti wa Jumuia ya Kitaifa ya wafanyabiasha Zanzibar ( ZNCC ) ndugu ALI AMOUR amesema lengo la ZNCC ni kuwajengea uelewa wa pamoja wafanyabiashara na wananchi juu ya matumizi sahihi ya mfumo wa Zanzibar Chamber Portal ambao utasaidia kuondoa changamoto na vikwazo vinavyoikabili Sekta ya Biashara na kuahidi kwamba ZNCC itaendelea kuwa daraja linalounganisha Serikali na sekta binafsi ikiongozwa na misingi ya ushirikiano na uwazi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Ndugu AMOUR amefahamisha kuwa sekta binafsi itaendelea kuwa mshirika wa maendeleo katika kuwekeza, kuzalisha, kuajiri, kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na kushiriki kikamilifu katika jitihada za kujenga uchumi imara na wenye ushindani.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiasha wenzake walioshiriki katika uzinduzi wa Mfumo wa ZPC Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Biashara la Zanzibar ( ZSTC ) Dkt. SOUD SAID ALI amesema uwepo wa mifumo ya kidijitali umerahisisha kufanya biashara kwa uwazi, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuwasilisha Serikalini changamoto na vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara wa Zanzibar.
Dkt. SOUD amesema usalama wa hali ya juu unahitajika katika uendeshaji wa mfumo huo ili kuepusha udukuzi wa taarifa na kushauri kupatiwa mafunzo watendaji watendaji wa ZNCC ili kuweza kufanyakazi kwa ufanisi zaidi



.jpeg)
No comments