WANANCHI UZI NA NG'AMBWA WALIA UWEKEZAJI HOTELI YA KITALII.
NaSaid Khamis
WANANCHI wa vijiji vya Uzi na Ng’ambwa, Wilaya ya Kati Unguja, wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro unaohusisha njia ya wananchi inayotumika kuelekea baharini, wakidai kuwa sehemu ya njia hiyo imezibwa na mwekezaji anayejenga hoteli ya kitalii katika eneo hilo.
Wakizungumza katika kikao cha kusikiliza kero za wananchi kilichofanyika kisiwani Uzi, wananchi hao walisema njia hiyo ni muhimu kwa shughuli zao za kila siku zikiwemo uvuvi, usafiri na shughuli nyingine zinazotegemea bahari, hivyo kuzibwa kwake kunasababisha usumbufu mkubwa kwa jamii.Kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kati, Rajab Ali Rajab, ameuagiza uongozi wa shehia za maeneo hayo kuhakikisha unasimamia haki na kufuata taratibu zote za serikali ili kutafuta suluhisho la haraka litakalolinda maslahi ya wananchi na wawekezaji kwa pamoja.
Amesema kuwa wananchi wa Kisiwa cha Uzi wanategemea kwa kiasi kikubwa rasilimali za bahari kwa shughuli zao za kiuchumi, hivyo ni muhimu suala hilo likafuatiliwa kwa karibu ili kuondoa sintofahamu na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya jamii na wawekezaji.
Rajab pia ameeleza kuwa serikali ina utaratibu maalumu wa kushughulikia masuala ya ardhi na maeneo yanayopitiwa na miradi ya maendeleo, ambapo tathmini hufanyika kabla ya utekelezaji wa miradi na fidia hulipwa kwa wahusika wote wanaostahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Mbali na suala hilo, wananchi wa Uzi na Ng’ambwa waliwasilisha changamoto nyingine zinazowakabili zikiwemo ukosefu wa gari la wagonjwa, kituo cha kulelea watoto, huduma za zimamoto na uokozi pamoja na vifaa vya ofisi kama mashine za printa na fotokopi, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kisiwa hicho
.jpeg)
maendeleo na yana gharama
ReplyDelete