Breaking News

MABOYA YAWEKWA MISALI KUIMARISHA UHIFADHI WA MATUMBAWE NA KUZUIA UVUVI HARAMU


Na Juma Seif.

Juhudi za kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa matumbawe ya baharini pamoja na uvuvi haramu katika Kisiwa cha Misali, Pemba, zimeendelea kuimarishwa kupitia uwekaji wa maboya ya kudumu katika eneo hilo muhimu la mazalia ya samaki.

Hatua hiyo imechukuliwa na Uhifadhi wa Mkondo wa Magharibi wa Bahari ya Hindi (PECCA) kwa lengo la kulinda mazingira ya bahari na kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinadumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja wa PECCA, Shafi Khamis Soud, alisema uwekaji wa maboya hayo hautaathiri shughuli za wavuvi, bali utasaidia kulinda maeneo muhimu ya mazalia ya samaki na hivyo kuongeza upatikanaji wa samaki katika maeneo ya uvuvi.

Alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya muda mrefu ya kuhifadhi bioanuwai ya bahari na kuimarisha uchumi unaotegemea rasilimali za baharini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ulinzi wa Kisiwa cha Misali, Haji Mohammed, alisema maboya hayo yatafungua njia ya kuimarisha usimamizi wa eneo hilo na kuwa alama muhimu katika utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu.



Alifafanua kuwa uhifadhi wa mazingira ya bahari ni nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya uvuvi na utalii, ambazo ni miongoni mwa sekta zinazochangia uchumi wa Zanzibar.

Wakati huo huo, wavuvi wametakiwa kuendelea kufuata sheria, kanuni na miongozo ya uvuvi ili kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa njia endelevu na inayolinda rasilimali za bahari.

Kisiwa cha Misali kinatajwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya mazalia ya samaki na matumbawe katika Mkoa wa Pemba, hivyo juhudi za uhifadhi zina umuhimu mkubwa katika kulinda mazingira na kuongeza uzalishaji wa rasilimali za baharini.




No comments