KAMATI YA UVUVI MZURI NA TASANI YAVUNJWA
Na Safia Mohamed.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, ameivunja Kamati ya Uvuvi ya Shehia za Mzuri na Tasani na kuagiza kufanyika kwa uchaguzi mpya wa viongozi.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kuibuka kwa malalamiko kutoka kwa wavuvi waliodai kuwa uchaguzi uliounda kamati hiyo haukufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, hali iliyosababisha migogoro ya mara kwa mara ndani ya jamii ya wavuvi.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Tasani, Hamida alisema lengo la hatua hiyo ni kurejesha utulivu, mshikamano na ufanisi katika sekta ya uvuvi ambayo ni chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa wananchi wa maeneo hayo.
Alisisitiza umuhimu wa uchaguzi mpya kufanyika kwa uwazi, haki na ushirikishwaji ili viongozi watakaochaguliwa waweze kupata ridhaa ya wanachama na kusimamia shughuli za uvuvi kwa amani na uwajibikaji.
Aidha, aliwataka wavuvi kudumisha umoja na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha migawanyiko wakati wakisubiri taratibu za uchaguzi mpya kukamilika.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Bahari Zanzibar, Mchanga Saidi aliwataka wavuvi kuweka pembeni tofauti zao na kuelekeza nguvu katika uhifadhi wa rasilimali za bahari.
Alisema usimamizi bora wa rasilimali za bahari unahitaji viongozi wanaokubalika na ushirikiano mzuri kati ya wavuvi na mamlaka husika ili kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali hizo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Baadhi ya wavuvi waliohudhuria mkutano huo walieleza matumaini yao kuwa uchaguzi mpya utaendeshwa kwa haki na uwazi, huku wakisisitiza kuwa hatua ya kuvunjwa kwa kamati ni mwanzo wa kurejesha imani, mshikamano na maendeleo katika sekta ya uvuvi ya Mzuri na Tasani.

No comments