VIONGOZI NA WANANCHI TUSHIKAMANE TUJENGE NCHI YETU ''OMO''
Na Siti Ali
Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, Leo Mei 08 2026, amejumuika na Waumini wa Kiislamu katika Sala ya Ijumaa hapo Msikiti wa Weles, Kikwajuni Mjini Unguja.
Akitoa salamu zake kwa Waumini na Wananchi waliofika hapo kumsikiliza, Alhaj Othman amesema Nguvu na Mafanikio ya Nchi yoyote Ulimwenguni, hutegemea Umoja na Mshikamano wa Kitaifa 'National Cohesion' baina ya Watu, Viongozi, na Jamii yote.
Alhaj Othman amekumbusha haja ya Wananchi kuwa Kitu- Kimoja na Kuimarisha Mshikamano katika Jamii na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo akikariri Hikma ya Mmoja wa Wanafalsafa Wakubwa Duniani, Ibnu Khalduun kupitia Kitabu chake cha 'MUQADDIMAH' kinachohimiza pia Maudhui ya Haja ya 'Mshikamano wa Kitaifa/Kijamii', katika kujenga Nchi na Taifa lenye-nguvu.
"Na katika hayo, sisi kama Waislamu tunayo mifano mingi", amesema akiitaja Ibada ya Hijja ambayo ni fursa na mfano adhim wa kuonyesha Mshikamano huo, unaotarajiwa kusaidia kuleta mageuzi katika nyanja zote za maisha, yakiwemo mabadiliko ya kitabia.
"Uislamu umetuletea neema kubwa sana kwetu, tunayo mambo mengi ya kutuleta pamoja na kutuweka katika mshikamano, umoja, kutambua wajibu wetu, uadilifu na kwamba sisi sote ni sawa Mbele ya Mwenyezi Mungu", ameeleza.
Amebainisha kushangazwa na baadhi ya Watu wanaokwenda kutekeleza Ibada Tukufu ya Hijja, bali kinyume chake hurejea badala ya kuhamasisha mema, huielekeza jamii kupinga maridhiano na mshikamano wa kuivusha Nchi kwenda katika mafanikio.
Amekumbusha Maneno ya Raia Mmoja wa Uingereza aliwahi kusema, Zanzibar siyo tu Nchi, bali ni Dhana ambayo imepita katika Misukosuko mingi, na imebaki ikidumu kuwa kitu kimoja, na Utambulisho wake na Watu wake.
Aidha amesisitiza kwamba yeye na Viongozi wa Chama chake, mbali na yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka jana, bado wamebaki wakipambania katika 'Asabia' wakiamini Zanzibar inahitaji mshikamano zaidi kulikoni baadhi ya Watu kulazimisha kujitwalia mamlaka.
Hivyo amesema ipo haja ya kujiuliza, hasa kwa Jamii za hapa Visiwani, na Tanzania kwa ujumla, iwapo Misingi hiyo ya 'Asabia' inawasaidia kama neema, katika kuyatawala Maisha ya Kila Siku, au vinginevyo.
Akitoa Khutba Mbili za Sala hiyo, Khatib Sheikh Ahmed Omar Abdallah, amesema ni wajibu kwa Waumini wa Kiislamu mwenye uwezo, kwenda Kuhiji katika Mji mtukufu Makkah, Ibada ambayo ni Nguzo ya Tano ya Uislam.
"Haya ni Maamrisho ya Mwenyezi Mungu, hivyo ni Wajibu kwetu kuyateketeza ipasavyo", amesisitiza Khatib huyo.
Mara baada ya Ibada hiyo Alhaj Othman amefika na kutoa Nkono wa Pole kwa Familia ya Marehemu Bi Fatma Salim Ahmed (Fatma-CUF), huko Kikwajuni Weles, pia ndani ya Mkoa wa Mjini- Magharibi Unguja.
Bi Fatma ambaye alikuwa ni Miongoni mwa Wanachama Waandamizi wa Harakati za Mageuzi Nchi, hadi akakumbukwa Mashuhuri kwa Jina la 'Bi Fatma CUF' akiungana Bega kwa Bega na Almarhum Maslim Seif Sharif Hamad katika Mapambano yake yote ya Kupigania Haki za Wananchi, alifariki-dunia mwishoni mwa Mwezi wa Aprili, Mwaka huu.
Viongozi mbali mbali wa Dini, Siasa na Jamii wameambatana na Mheshimiwa Othman katika Ibada hiyo, wakiwemo Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho Mhe. Omar Said Shabani; na Katibu wa Idara Habari na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ndugu Salim Biman

.jpeg)

No comments