Breaking News

VIJANA WATAKIWA KUBADILI MIENENDO KUEPUKA MAMBUKIZI MAPYA YA VVU UNGUJA.

 


Na Said Khamis.

Jamii imetakiwa kubadili tabia na kujiepusha na vishawishi hatarishi ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU, hasa miongoni mwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa. Wito huo umetolewa na Ofisa wa Afya Wilaya ya Kati Unguja, Ali Sharif Mohamed, wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyofanyika Dunga TC kwa vijana wa mabaraza ya vijana kutoka shehia mbalimbali.

Akizungumza katika mafunzo hayo, alisema takwimu zinaonesha kuwa Wilaya ya Kati inaongoza kwa maambukizi mapya ya VVU kwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 26 ikilinganishwa na Wilaya ya Kusini Unguja. Hali hiyo, alisema, inahitaji juhudi za pamoja za kubadili mienendo na kuongeza uelewa wa vijana juu ya hatari zinazowakabili.

Alifafanua kuwa baadhi ya sababu zinazopelekea kuongezeka kwa maambukizi ni pamoja na starehe zisizo na mipaka, kushiriki ngoma za usiku na matumizi ya pombe kupita kiasi. Alieleza kuwa mazingira hayo huondoa umakini na kuwafanya vijana kujikuta wakijihusisha na vitendo hatarishi.



Kwa upande wake, Daktari wa Ushauri Nasaha kutoka Kituo cha Afya Mwera, Issa Abdalla Issa, aliwataka vijana kuacha tabia ya kusubiri kupima afya zao kabla ya kufunga ndoa. Alionya kuwa kufanya hivyo ni hatari kwa kuwa maambukizi ya VVU yanaweza yasigundulike mapema kutokana na dalili kuchelewa kuonekana.

Aidha, aliwahimiza vijana kutumia vituo vya huduma rafiki vilivyopo ili kupata elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi na njia za kujikinga. Alibainisha kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo UKIMWI, saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti.

Akizungumza kwa niaba ya vijana, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wilaya ya Kati, Daudi Suleiman Haji, alisema mafunzo hayo yatawasaidia kubadili mtazamo na kuchukua hatua sahihi za kujilinda. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji kwa ufadhili wa UNICEF, yakilenga kuimarisha afya na ustawi wa vijana.


No comments