SMZ YAPOKEA MILIONI 500 KUJENGA VITUO VYA KULELEA WATOTO MASOKONI
Na Said Khamis
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepokea hundi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kulelea watoto katika maeneo ya biashara, hususan masokoni, ikiwa ni hatua ya kuboresha ustawi wa watoto na kuwawezesha kina mama wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa utulivu zaidi. Mpango huo unalenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya kukosekana kwa maeneo salama ya kuwaacha watoto wakati wa kazi, jambo lililokuwa likiwaathiri wazazi na watoto kwa pamoja.
Akizungumza wakati wa kupokea hundi hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa, alisema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha watoto wanapata malezi bora tangu wakiwa wadogo. Alifafanua kuwa uwepo wa vituo hivyo utasaidia kukuza maendeleo ya watoto kimwili na kiakili, sambamba na kuwajengea msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
Alieleza kuwa kina mama wengi wanaofanya biashara katika masoko wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuwahudumia watoto wao wanapokuwa kazini, hali inayowalazimu ama kuwabeba watoto katika mazingira yasiyo rafiki au kuwaacha katika mazingira hatarishi. Hivyo, ujenzi wa vituo hivyo utakuwa suluhisho muhimu litakalowawezesha wazazi kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Waziri huyo alisema Serikali imeandaa programu maalum ya miaka mitano itakayohakikisha vituo vya kulelea watoto vinajengwa katika masoko mbalimbali nchini, ambapo hatua ya awali ya utekelezaji itaanza katika eneo la Soko la Mwanakwerekwe. Alisisitiza kuwa juhudi hizo zinaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, lishe sahihi na mazingira salama ya kukua.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul, aliipongeza Serikali na wadau kwa kuanzisha mpango huo, akisema kuwa vituo hivyo vitatoa fursa kwa watoto kuwa katika mazingira salama na rafiki. Aliongeza kuwa wazazi, hasa kina mama, watanufaika kwa kupata nafasi ya kuwanyonyesha watoto wao wanapohitajika bila kuathiri shughuli zao za kiuchumi.
Alieleza kuwa kupitia mpango huo, Serikali inalenga kuwahudumia watoto kuanzia umri wa miaka sifuri hadi minane, hatua itakayochangia kwa kiasi kikubwa kukuza malezi bora katika hatua za awali za maisha ya mtoto. Aidha, alisema vituo hivyo vitasaidia kupunguza vitendo vya udhalilishaji vinavyoweza kujitokeza kwa watoto wanaokosa uangalizi katika mazingira yasiyo salama.
Naye Mratibu wa Programu Jumuishi ya Malezi na Makuzi ya Mtoto Zanzibar, Mariam Mussa, alisema utafiti uliofanywa umebaini kuwa watoto wengi wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuishi katika mazingira yasiyo salama na yasiyozingatia maadili. Alieleza kuwa katika maeneo ya masoko, watoto hukumbana na mienendo isiyofaa na matumizi ya lugha chafu ambayo inaweza kuathiri makuzi yao.
Kutokana na hali hiyo, alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa vituo maalum vya kulelea watoto ili kuwalinda dhidi ya mazingira hatarishi na kuwapatia malezi yanayozingatia maadili na usalama wao. Aliongeza kuwa vituo hivyo vitakuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi za ulinzi na malezi bora.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Stanbic Bank, Derick Lugemala, alisema taasisi yao imeamua kushirikiana na Serikali katika mradi huo kwa kutambua umuhimu wake kwa jamii. Alibainisha kuwa ushirikiano huo unalenga kusaidia kina mama wafanyabiashara na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Save the Children, Angela Kaulen, aliishukuru Serikali kwa kuanzisha programu hiyo ya kitaifa, akisema ni hatua muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi. Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali ni nguzo muhimu katika kufanikisha jitihada za kulinda na kukuza ustawi wa mtoto.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo Stanbic Bank, Save the Children pamoja na PDB, ukiwa na lengo la kujenga jamii yenye ustawi bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo, huku ukihakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, yenye kuzingatia maadili na maendeleo yao kwa ujumla.



No comments