KAA TOPE KUFANYIWA UTAFITI ZANZIBAR KUBORESHA UVUVI.
Na Said Khamis.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza rasmi mchakato wa kufanya utafiti wa kina kuhusu uvuvi wa kaa tope, hatua inayolenga kuimarisha sekta ya uvuvi na kuhakikisha inakuwa endelevu huku ikichangia kikamilifu katika uchumi wa buluu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wataalamu na wadau wa sekta hiyo uliofanyika Maruhubi, Wilaya ya Mjini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Zahor Kassim Alkharous, amesema utafiti huo utasaidia kubaini hali halisi ya uzalishaji, changamoto zinazokabili sekta pamoja na fursa zilizopo.
Amesema licha ya uvuvi wa kaa tope kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi, bado kuna haja ya kuwa na takwimu sahihi na utafiti wa kina utakaosaidia kuboresha usimamizi wa rasilimali hiyo, kuongeza tija na kuwezesha maamuzi bora ya kisera na kiutendaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Zanzibar (ZAFIRI), Dk. Zakaria Ali Khamis, amesema mkutano huo umeweka msingi muhimu wa utafiti huo, ambao utachunguza mwenendo wa uvuvi wa kaa tope kwa kuangalia kiwango cha uzalishaji, mbinu zinazotumika pamoja na changamoto zinazowakabili wavuvi.
Ameongeza kuwa utafiti huo pia utazingatia umuhimu wa kutumia mbinu bora za uvuvi endelevu ili kulinda rasilimali za baharini na kuhakikisha sekta hiyo inanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Wadau mbalimbali walioshiriki katika mkutano huo wameeleza kuwa sekta ya uvuvi wa kaa tope inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uharibifu wa mazingira ya mikoko, ukosefu wa elimu kuhusu uvuvi endelevu, pamoja na uhaba wa masoko ya uhakika kwa bidhaa hiyo.
Mkutano huo uliwakutanisha wataalamu kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Tanga, wawakilishi wa vyuo vikuu pamoja na wavuvi wa kaa tope. Washiriki walikubaliana kuwa utafiti huo ufanyike katika maeneo yote ya pwani na uhusishe ukusanyaji wa takwimu sahihi pamoja na ushirikishwaji wa jamii za wavuvi.
Hatua hii inaonekana kuwa mwanzo muhimu wa juhudi za kuifanya sekta ya uvuvi wa kaa tope kuwa yenye tija zaidi, rafiki kwa mazingira, na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa buluu Zanzibar.




No comments