WENYE UWEZO WATAKIWA KUFTARISHA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN.
Na Said Khamis.
Vikundi vya ushirika pamoja na taasisi mbalimbali zenye uwezo zimetakiwa kuendelea kutoa msaada kwa watoto yatima na watu wanaoishi katika mazingira magumu, hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Wito huo umetolewa na Diwani wa Viti Maalum kutoka Wilaya ya Dimani, Maryam Salehe Ali, wakati akizungumza katika hafla ya iftar iliyoandaliwa na Kikundi cha Amani na Upendo kinachofanya shughuli zake katika eneo la Michenzani Mall. Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa ZSSF Kariakoo, Mjini Unguja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Maryam alisema kuwa watu wenye uwezo wana jukumu la kijamii la kuwasaidia na kuwafariji watoto yatima kwa hali na mali, ili nao wajisikie kuwa na haki sawa kama watoto wengine katika jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Amani na Upendo, Husna Mkuja Suleiman, alisema kuwa lengo la kuandaa iftar hiyo ni kuwafariji watoto yatima na kuwapa faraja, kwani wengi wao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika maisha yao ya kila siku.
Aliongeza kuwa kupitia shughuli kama hizi, jamii inapata fursa ya kuonesha mshikamano na upendo kwa makundi yenye uhitaji zaidi.
Baadhi ya watoto yatima walioshiriki katika iftar hiyo walitoa shukrani zao kwa kuandaliwa kwa futari hiyo na kuomba wananchi pamoja na wahisani mbalimbali kuendelea kuwasaidia kwa hali na mali ili kuboresha maisha yao.
Hafla hiyo ya iftar iliandaliwa na Kikundi cha Amani na Upendo na kuwashirikisha watoto yatima, wanakikundi pamoja na wananchi wengine mbalimbali walioungana katika kuonesha upendo na mshikamano katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.


No comments