Breaking News

RIPOTI YA 2025 YAIBUA CHANGAMOTO ZA UHURU WA HABARI ZANZIBAR.



Na Mwandishi wetu.

Mashirika ya habari na haki za binadamu Zanzibar yametoa ripoti ya ufuatiliaji wa mwaka 2025 inayobainisha mafanikio na changamoto katika sekta ya habari, hususan katika kipindi cha uchaguzi.

Ripoti inaonesha kuwa licha ya kuimarika kwa uwezo wa waandishi wa habari kupitia mafunzo mbalimbali, bado kulikuwepo na ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari. Waandishi wengi waliegemea zaidi kauli za viongozi wa kisiasa huku makundi ya pembezoni kama wanawake, vijana, wazee na jamii za vijijini yakipewa nafasi ndogo katika taarifa za habari.

Aidha, mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari hayakuwa rafiki, yakijumuisha vitisho, unyanyasaji, kunyimwa taarifa na kulazimishwa kufuta maudhui, hasa katika habari za uchaguzi na uwajibikaji. Vyombo vya habari vya mtandaoni vilikumbwa zaidi na barua za onyo na vitisho vya kufutiwa leseni.



Ripoti pia imebaini changamoto za kisheria zinazotokana na sheria za habari zilizopitwa na wakati, pamoja na upendeleo wa vyombo vya habari vya serikali katika kipindi cha uchaguzi, hali iliyodhoofisha uwazi na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi.

Kutokana na hali hiyo, mashirika yametoa wito kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya marekebisho ya haraka ya sheria za habari, kulinda uhuru wa waandishi wa habari na kuhakikisha mazingira huru na salama ya utendaji wa vyombo vya habari kama nguzo ya demokrasia na utawala bora


No comments