Breaking News

ZANZIBAR YAPIGA HATUA KUBWA KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA UKIMWI, KIWANGO CHASHUKA CHINI YA ASILIMIA MOJA.

Na Siti Ali


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya Ukimwi kwa zaidi ya miongo mitatu na kufanikiwa kushusha kiwango cha maambukizi hadi chini ya asilimia moja.

Mhe. Hemed alitoa kauli hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, alisema kuwa Zanzibar imepunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi mapya kutoka watu 362 (mwaka 2020) hadi kufikia watu 211 (mwaka 2025). Aidha, vifo vitokanavyo na Ukimwi vimeshuka kutoka 230 (2020) hadi 115 (2025), hatua inayodhihirisha mafanikio ya wazi ya mapambano hayo.

Mhe. Hemed alifafanua kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa Mpango Endelevu wa Kupambana na Ukimwi Zanzibar, wenye lengo la kuhakikisha mapambano yanaendelea kwa ufanisi hadi kufikia malengo ya kumaliza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda na kusimamia Sheria na Sera zote bila ubaguzi ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wote bila kuwekwa pembeni. Pamoja na mafanikio hayo, alitaja changamoto zinazoendelea kushuhudiwa ikiwemo upungufu wa rasilimali fedha, unyanyapaa na tabia hatarishi miongoni mwa vijana, ambazo zinahitaji nguvu ya pamoja.

Katika kuunga mkono jitihada za watu wanaoishi na VVU, Mhe. Hemed ameihakikishia Jumuiya ya ZAPHA+ kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi itashughulikia changamoto zao, ikiwemo kuongeza bajeti ya dawa za ARV, vipimo, na kuwezesha harakati za mapambano dhidi ya Ukimwi.



Amesisitiza umuhimu wa jamii kutoendeleza unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU kwani kufanya hivyo kunadhoofisha jitihada za kupunguza maambukizi mapya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ukimwi Zanzibar, Dkt. Ali Salim Ali, alisema kuwa juhudi za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zimefanikiwa hadi kiwango kilicho chini ya asilimia mbili hatua muhimu inayoiweka Zanzibar karibu na lengo la kutokomeza kabisa maambukizi hayo.

Ameeleza kuwa programu za kuwafikia makundi maalum zimeimarishwa ambapo jumla ya watu 6,421 wamepata elimu, ushauri nasaha, upimaji na huduma za tiba Unguja na Pemba. Pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha wanaume wanapata huduma za VVU bila vikwazo.

Katika risala ya watu wanaoishi na VVU, Bi. Sara Abdi Mwita aliiomba Serikali kuweka dawa za ARV kwenye bajeti yake ya moja kwa moja kutokana na kusuasua kwa baadhi ya wafadhili. Pia ameomba kuwepo na mfumo wa utambuzi katika vituo vya huduma ili kuondoa usumbufu wanaoupata wakati wa kutafuta huduma muhimu.

Ameishauri Serikali kuanzisha mfuko maalumu wa HIV kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za ufadhili na kuhakikisha huduma za msingi zinapatikana kwa watu wote wanaoishi na VVU.

Siku ya Ukimwi Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 1 Disemba, na kaulimbiu ya mwaka 2025 ni

“TUVISHINDE VIKWAZO VYA KISERA, TUIMARISHE MAPAMBANO YA UKIMWI.


No comments