Breaking News

USHIRIKIANO WA SERIKALI NA WADAU CHACHU UFANISI.



Na Said Khamis

Mashirikiano ya karibu kati ya Serikali, wakandarasi na Benki ya NMB yametajwa kuwa nguzo muhimu ya kuhakikisha miradi ya Serikali inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, wakati akifungua semina maalum ya mafunzo kwa wakandarasi iliyoandaliwa na Benki ya NMB ambayo imefanika  katika Hoteli ya Verde, Wilaya ya Magharibi A, Unguja.

 Dkt. Khalid amesisitiza kuwa NMB inapaswa kuwa mshauri mkuu katika masuala ya kifedha, huku akiwataka wakandarasi wa ndani kushirikiana kwa pamoja ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuimarisha sekta ya miundombinu.

Aidha, amewahimiza wakandarasi kufuatilia na kutumia kikamilifu fursa zilizopo, pamoja na kuzingatia uzalendo, akibainisha kuwa miundombinu inayotekelezwa ni mali ya wananchi na inalenga kuboresha maisha yao.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya Serikali inatekelezwa kwa wakati uliopangwa na kwa manufaa mapana kwa jamii.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Mhe. Badria Atai Masoud, amewapongeza wadau wa Benki ya NMB kwa kuwa na wigo mpana wa huduma zinazowagusa wananchi, huku akiwataka kuongeza bidii katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha wananchi wanapata msaada kwa wakati unaofaa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, amesema benki hiyo imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuunga mkono maendeleo ya sekta ya ujenzi kupitia utoaji wa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo mikopo maalum kwa wakandarasi.

Ameongeza kuwa NMB imeboresha huduma za Internet Banking na NMB Mkononi ili kurahisisha miamala, ufuatiliaji wa fedha na usimamizi wa kifedha kwa njia ya kidijitali, kwa usalama na wakati wowote bila ulazima wa kufika tawi la benki.


No comments