Breaking News

UJENZI WA KITUO CHA AFYA TUMBATU KUKAMILIKA MACHI 2026, HUDUMA ZA MAMA NA MTOTO NA DHARURA KUTOLEWA.

 


Na Siti Ali

Kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha Afya Tumbatu, kutaimarisha  kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za afya za msingi ikiwemo huduma za  mama na mtoto, huduma za dharura, maabara pamoja na huduma za kinga na tiba

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla wakati wa  uwekaji wa Jiwe na Msingi la kituo cha Afya Tumbatu ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema uamuzi wa kujengwa kituo hichi cha afya ni hatua muhimu ya Serikali katika kuimarisha miundominbu ya afya, ili kuhakikisha  wananchi wote wanapata huduma kwa ukaribu katika mazingira bora myanayolingana na viwango vya kimataifa na kuweka mazingitio maalum kwenye maeneo ya visiwa katika utoaji na upatikanaji wa huduma zote zinazohitajika.

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Serikali inaendelea na shabaha yake ya kuweka mifumo imara katika Sekta ya afya, ikiwema mfumo wa rufaa ambapo tayari  imekamilisha ujenzi wa Hospitali za Wilaya zinaendelea kutoa huduma kwa wananchi katika Wilaya zote za Zanzibar.



Aidha, amefahamisha kuwa hatua inayoendelea sasa ni ujenzi wa Hospitali za Mikoa katika mikoa minne iliyobaki, ujenzi wa Hospitali kubwa na ya kisasa ya Binguni  pamoja na kuifanyia matengenezo makubwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambapo hospitali ya Mkoa ya Lumumba inaendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais ameuagiza uongozi wa Wizara ya afya kuhakikisha kipaombele cha ajira wanapewa vijana wazawa wenye sifa na uwezo wa kutoa huduma za afya, kuwepo kwa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) na  wataalamu wa kutosha watakaotoa huduma za dhurura kwa masaa 24, ili kuhakikisha huduma za uhakika za dharura kwa mama wajawazito na wagonjwa wengine wa dharura zinapatikana kuanzia ngazi ya jamii, kituo cha Afya na Hospitali.

Katika hafla hio Mhe. Hemed amewaelekeza Mkandarasi na wasimamizi wa mradi huu wa Kituo cha Afya Tumbatu, kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati uliopangwa na kuzingatia viwango vya ubora vinavyokubalika pamoja na kuwasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wasimamizi na wakandarasi hao kwa kuilinda na kuitunza miundombinu hio ili iweze kutunufaisha sisi na vizazi vijavyo.

Amewataka Wazanzibari kuendelea kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi yetu Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, kudumisha amani na mshikamano ambao ndio nyenzo muhimu katika kuyafikia maendeleo wanayoyatarajia.



Akisoma taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa mradi wa kituo cha Afya Tumbatu, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya inaendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2025-2030 ibara ya 93 na ahadi za Mhe. Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dr. Hussein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha wanaimarisha sekta ya Afya kwa lengo la kuboresha ustawi wa jamii na kupunguza vifo vinayotokana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyokuambukiza.

Amesema katika kufikia malengo hayo, wizara imejikita kwenye utekelezaji wa vipaombele vitano vya serikali katika kuimarisha huduma za Afya ya msingi kwa jamii ambavyo ni kuwa na Miundombinu rafiki kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuwa na  watumishi wenye sifa na uwezo wa kutoa huduma kwa wakati, upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba pamoja na utoaji wa huduma za Afya kwa kutumia mifumo ya Tehama.

Dkt. Mngereza amefahamisha kuwa Ujenzi wa Kituo cha afya Tumbatu utakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wakaazi wa Shehia zote za Tumbatu ambao ni zaidi ya watu 18,366 ambapo kitakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa zaidi ya 30 kwa wakati mmoja na kutoa huduma kwa masaa 24 ya kazi.

Aidha kituo cha Afya Tumbatu kinatarajiwa kutoa huduma za Klinik na wagonjwa wa nje (OPD), huduma za Klinik za mama na mtoto, huduma za magonjwa ya dharura na ajali, uchunguzi wa maradhi mbali mbali pamoja na huduma za wagonjwa wa Upasuaji (Operating Theatre).



Mradi wa kituo cha Afya Tumbatu unajengwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 6.4 chini ya Mkandarasi SIMBA DEVELOPER  LTD na kInasimamiwa na Kampuni ya Health Care Engineering and Infrastructure Department unaotarajiwa kukamilika mwezi Machi 2026.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Cassian Gallos Nyimbo ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuliangalia kwa umakini suala la Kisiwa cha Tumbatu kuwa Wilaya inayojutegemea kutokana na ongezeko la watu wanaoishi wilayani hapo jambo linalohitaji kuongezeka kwa huduma mbalinmbali za kiuchumi na kijamii. 

Mhe. Nyimbo amesema kuna uhitaji wa kujengwa kwa soko kubwa na la kisasa katika kisiwa ya Tumbatu ili kukifungua zaidi  kisiwa hicho kibiashara na kukuza uchumi kwa wananchi wa Kisiwani humo na Mkoa wa kaskazini Ungaja kwa ujumla.


No comments