Breaking News

RWANDAIR YAANZA SAFARI ZA KIGALI–ZANZIBAR, KUKUZA UTALII NA BIASHARA .

 


Na Said Khamis.

SERIKALI ya Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi imeendelea kuhakikisha mazingira bora ya utendaji wa kazi za usafiri wa anga, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa weledi na ufanisi.

 Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Seif Abdallah Juma, wakati wa hafla ya mapokezi ya safari ya kwanza ya RwandAir kutoka Kigali kwenda Zanzibar iliyofanyika jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Akizungumza katika hafla hiyo, Seif alisema ujio wa ndege hiyo umetokana na mazingira wezeshi ya huduma za anga yaliyopo Zanzibar, ikiwemo upanuzi wa viwanja, ujenzi wa majengo mapya ya abiria na miundombinu imara inayokidhi mahitaji ya kimataifa. Alibainisha kuwa mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya anga kati ya pande hizo mbili yalikuwa ya muda mrefu na kutua kwa ndege hiyo kulikuwa ndoto iliyotimia kwa pande zote.

Alisema hatua ya RwandAir kuanzisha safari za Zanzibar ni fursa muhimu ya kukuza utalii, uchumi na biashara, huku akisisitiza kuwa Warwanda ni ndugu wa Watanzania na majirani wa karibu wanaochangia kwa pamoja katika ukuaji wa uchumi wa kikanda. 

Aidha, alibainisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo salama, hakuna vurugu na ujio wa ndege hiyo ni uthibitisho wa hali hiyo, akisema matarajio ya mamlaka ni kuona Zanzibar ikiendelea kuongoza kwa idadi ya ndege zinazoingia ndani ya mwezi huu Desemba.

Kwa upande wake, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Patrick Nyamvumba, alisema uzinduzi wa safari hiyo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Rwanda, hususan katika masuala ya biashara, utalii, uhamaji wa watu na maendeleo ya kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Alisema kuunganika kwa Zanzibar na Kigali kutafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na kubadilishana tamaduni na ni hatua muhimu katika kuongeza mchango wa Afrika kwenye sekta ya utalii duniani.



Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa RwandAir, Ernest Mushi, alisema Zanzibar imekuwa kituo cha tatu cha shirika hilo nchini Tanzania baada ya Dar es Salaam na Kilimanjaro na kuanzishwa kwa safari hizo kunalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za anga kwa ufanisi na urahisi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema safari hizo zitawaunganisha wasafiri kati ya Kigali, Zanzibar na Mombasa kwa urahisi zaidi kupitia mtandao mpana wa safari za RwandAir.

 Ndege hiyo imeanza safari zake  Zanzibar kwa mara ya kwanza ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 109 huku safari zake zikitarajiwa kufanyika mara nne kwa wiki, Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili.


No comments