SERIKALI KUFANYA MABADILIKO YA MITAALA YA ELIMU SEKONDARI, KUENDANA NA KASI YA TEKNOLOJIA.
Na Said Khamis
WAZIRI wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif Alwardy, amesema serikali inaendelea kutekeleza mageuzi ya elimu, ikiwemo mabadiliko ya mtaala wa sekondari ili kuendana na mabadiliko ya kijamii, kiteknolojia na kiuchumi yanayoendelea duniani.
Aliyasema hayo katika ufunguzi wa skuli ya sekondari Tunguu, Mwenge, Chuini, Mbuzini na Koani, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi, hafla iliyofanyika Tunguu mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema utekelezaji wa mtaala mpya unahitaji kuwepo miundombinu ya kisasa, mazingira rafiki ya ufundishaji na ujifunzaji, vifaa stahiki pamoja na walimu wenye weledi na ujuzi wa kisasa.
Aidha alisema hatua hiyo ni kielelezo cha utekelezaji wa mageuzi ya elimu yanayoakisi mabadiliko ya mtaala wa elimu ya sekondari unaolenga ujifunzaji wa vitendo, ujengaji wa ujuzi na kukuza ubunifu.
"Ujenzi wa skuli hizi ni maono ya serikali ya kuwekeza katika miundombinu rafiki na ya kisasa itakayowezesha utekelezaji wa mtaala mpya kwa ufanisi" alisema
Alifahamisha kuwa mageuzi ya elimu yanaendelea kuwa chachu ya ujengaji wa rasilimali watu imara na nguzo muhimu ya kufanikisha malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya Zanzibar, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.
Akizungumzia miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema serikali inaendelea kuenzi na kutafsiri falsafa ya Mapinduzi kwa vitendo ikiwemo kuekeza katika sekta ya elimu kwa kuimarisha upatikanaji wa elimu na kuhakikisha miundombinu na mifumo ya elimu inaendana na mahitaji ya sasa na baadaye kwa maendeleo ya Taifa.
"Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliweka elimu kuwa haki ya msingi kwa watoto wote bila kujali asili, eneo au hali ya maisha na yakaifanya elimu kuwa nyenzo kuu ya kumkomboa mwananchi dhidi ya ujinga, umaskini na utegemezi" alisema.
Sambamba na hayo aliwataka wananchi kushirikiana na uongozi wa skuli kuhakikisha miundombinu hiyo inatunzwa vizuri ili kuwezesha vizazi kuendelea kufaidika na miundombinu ya kisasa kwa muda mrefu.
Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khadija Salum Ali alisema majengo hayo ni matunda ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yanayotokana na Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.
Aidha alisema viongozi wa wizara hiyo wana kila aina ya sababu ya kuzungumzia maendeleo yanayoendelea nchini hususan katika sekta ya elimu ambayo yametekelezwa kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 na 2025 2030.
Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kuifanya sekta ya elimu kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake na kutoa nyenzo kila uchao ili kukamilisha malengo yaliyowekwa.
Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mradi wa ujenzi wa skuli tano, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Amos John Henock alisema ujenzi huo umegharimu shilingi bilioni saba ambapo kila skuli imegharimu zaidi ya shilingi bilioni Moja.
Alifahamisha kuwa ujenzi huo ulianza Septemba 2024 na kukamilika Disemba 2025 ambapo kila skuli ina madarasa 8 vyoo 19, chumba cha ushauri nasaha, maabara 2, chumba cha TEHAMA, Maktaba Ofisi za walimu huku kila skuli inaweza kuchukua wanafunzi 360 kwa wastani wa wanafunzi 45 kwa darasa.
Akitoa salamau za mkoa huo Mkuu wa wilaya ya Kati Unguja, Rajab Ali Rajab aliomba wizara hiyo kuangalia namna ya kujengewa skuli nyengine za ghorofa katika wilaya hiyo kama zilivyo wilaya nyengine kwani mpaka sasa imebahatika skuli moja ya ghofa.
.jpeg)

.jpeg)

No comments