Breaking News

FUONI KUNUFAIKA NA KITUO CHA AFYA CHA KISASA



Na Siti Ali

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kujenga kituo cha  Afya kikubwa cha kisasa katika Jimbo la Fuoni.

Ameyasema hayo katika hafla ya ufungaji wa kampeni za CCM za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Fuoni unaotarajiwa kufanyika Disemba 30 2025zilizofanyika katika uwanja wa mpira fuoni.

Amesema Mkandarasi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Fuoni anatarajiwa kuanza kazi wakati wowote kuanzia sasa kwa kujengwa kituo kikubwa cha kisasa kitakachotoa huduma za matibabu kwa wananchi wengi zaidi.

Akizungumzia ujenzi wa miundombinu ya barabara Mhe. Hemed ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani amesema katika Jimbo la Fuoni Serikali imejenga barabara mbali mbali ambazo zipo zilizokamilika na zilizofikia hatua ya kuwekwa lami zitakazokwenda kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji ndani ya Jimbo la Fuoni.



Amefahamisha kuwa Serikali imetekeleza vyema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika suala zima la ujenzi wa miundombinu ya skuli ambapo kwa sasa ujenzi wa skuli ya Msingi Fuoni kibondeni inayojengwa ya Ghorofa (G+2) umeanza rasmi.

Makamu wa Pili wa Rais  amesema  ujenzi wa nyumba za kisasa unaendelea katika eneo la Fuoni Kibondeni (Kisakasaka) ambapo kutakuwa na miradi mitatu ambayo ni Kisakaka A yenye idadi ya nyumba 240, kisakasaka B idadi ya nyumba 548 na kisakasaka D idadi ya nyumba 312 ambazo asilimia 40 ya kila mradi zitakodishwa kwa watu wenye kipato cha chini na asilimia 60 zitauzwa na kukopeshwa kwa watu ambao watalipa kidogo kidogo ili kila mtu anufaike na miradi hio kama agizo la Mhe. Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi linavyoelekeza.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed  ametumia hadhara hio kwa kumnadi na kumuombea kura mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Fuoni ndugu Asha Hussein Saleh kwa kusema mgombea huyo ana sifa zote za kuwa mbunge wa Jimbo la Fuoni na anaweza kuwatumikia akiwa anatambua changamoto zilizomo jimboni humo hivyo  amewataka wananchi wa ifikapo tarehe 30 disemba kumchagua kwa kura nyingi mgombea huyo ili aweze kuwatumikia.



Katibu wa Idara ya Siasa, Itikadi, Uwenezi na Mafunzo ya Chama cha Mapinduzi komred Khamis Mbeto Khamis amesema kampeni za uchaguzi katika jimbo la Fuoni zimefanyika vizuri na muitikio wa wa wanaCCM na wannachi kwa ujumla ulikuwa mkubwa ambapo Mgombea wa Ubunge katika Jimbo hilo aliinadi vyema Ilani ya CCM na kusema kuwa Jimbo hilo litaendelea kushikiliwa na Chama cha Mapinduzi.

Komred Mbeto amesema Serikali ya Awamu ya Nane (8) inayoongozwa na Rais Dkt Hussein Mwinyi imetekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM kwa kujenga miradi mbali mbali ya Maendeleo ambapo Jimbo la Fuoni ni wanufaika wa miradi hio hivyo wanayo sababu ya kuipigia kura CCM ili iendelee kuitekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030.

Kwa upande wake Mgombea wa Ubunge Jimbo la Fuoni ndugu Asha Hussein Saleh ametumia hadhara hio kuomba kura kwa wananchi wa Fuoni ambapo amesema akipata ridhaa ya kuwa mbunge wa Jimbo hilo  anaahidi kuitekeleza vyema Ilani Ya CCM kwa kuwatumikia nankuzitatua changamoto zilizomo ndani ya Jimbo la Fuoni .

Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Fuoni unaotarajiwa kufanyiaka Disemba 30, 2025 unafanyika kufuatia kifo cha Mbunge mstaafu na aliyekuwa mgombea wa Ubunge wa Jimbo hilo kwa Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi marehem Abass Ali Mwinyi.


No comments