Wanasayansi Wagundua Uwezekano wa Umeme Katika Anga la Sayari ya Mars.
Kwa mara ya kwanza katika historia, wanasayansi wanaamini wamefanikiwa kurekodi shughuli za umeme katika anga ya sayari ya Mars, jambo linaloashiria kuwa sayari hiyo inaweza kuwa na umeme unaofanana na radi.
Rover ya Perseverance ya NASA, iliyotua kwenye Mars mwaka 2021 kwa lengo la kutafuta viashiria vya uhai, imetumia miaka minne iliyopita kuchunguza eneo la Jezero Crater. Katika uchunguzi huo, kifaa chake kiitwacho SuperCam kimerekodi sauti na mawimbi ya sumakuumeme yaliyoonyesha kuwepo kwa kile kinachoitwa “mini lightning”—umeme mdogo unaojitokeza kwenye anga.
Umeme Utokanao na Vimbunga vya Vumbi
Timu ya watafiti kutoka Ufaransa ilichambua zaidi ya saa 28 za rekodi za sauti zilizotolewa na rover hiyo katika kipindi cha miaka miwili ya Mars (sawa na siku 1,374 za Dunia). Matokeo yao yalionyesha kuwa umeme huo mdogo mara nyingi hutokea wakati wa:
-
Vimbunga vya vumbi (dust devils)
-
Mbeleko za dhoruba za vumbi (dust storm fronts)
Dust devils ni viringi vidogo vya upepo vinavyotokana na hewa ya moto kupanda juu kutoka ardhini. Mizunguko yake ya ndani inaweza kusababisha mgongano wa chembe za vumbi na hatimaye kuzaa umeme.
Ugunduzi Mkubwa Kwa Mustakabali wa Uchunguzi wa Mars
Dk. Baptiste Chide, mwandishi kiongozi wa utafiti huo, aliambia Reuters kuwa discharges hizo ni “ugunduzi mkubwa wenye athari za moja kwa moja kwa kemia ya anga ya Mars, hali ya hewa, uwezekano wa makazi ya viumbe hai, na safari zijazo za roboti na binadamu”.
Kwa mujibu wa wanasayansi hao, Mars sasa inajiunga na Dunia, Saturn na Jupiter—sayari zinazojulikana kuwa na shughuli za umeme angani.
Hata hivyo, bado kunayo changamoto. Dk. Daniel Pritchard, mwanafizikia wa chembe, aliandika kwenye jarida la Nature kuwa, ingawa sauti zilizorekodiwa zinatoa ushahidi mzito wa umeme huo unaosababishwa na vumbi, ukweli kwamba haujaonekana moja kwa moja kwa macho unafanya mjadala kuendelea.
Je, Maisha Yaliwahi Kuwapo Mars?
Mnamo Septemba mwaka huu, wanasayansi waligundua mawe yenye alama za ajabu kwenye Marsyaliopewa majina kama “leopard spots” na “poppy seeds”. Mawe haya yana madini yaliyotokana na michakato ya kemikali ambayo huenda ina uhusiano na vijidudu vya kale.
Ingawa madini hayo yanaweza pia kuwa matokeo ya michakato ya kijiolojia, NASA imesema kuwa alama hizo ndizo dalili zilizo wazi zaidi kufikia sasa kuashiria uwepo wa maisha ya zamani.
Kwa sasa Mars ni jangwa baridi lisilo na unyevu, lakini ushahidi unaonyesha kuwa mabilioni ya miaka iliyopita ilikuwa na anga nene na maji ya kutiririka—mazingira muafaka kwa maisha.
Perseverance ilipelekwa katika Jezero Crater kwa sababu eneo hilo linaonyesha kuwa huenda lilikuwa delta ya mto, kipindi ambacho Mars ilikuwa na uwezo wa kubeba maji juu ya uso wake, ikiashiria uwezekano wa maisha ya kale.

No comments