WADAU WA MICHEZO WATAKA CHANGAMOTO ZA WATOTO WA KIKE ZITATULIWE ILI KUWAPA UHURU KUSHIRIKI MICHEZO
MICHEZO ni sehemu muhimu ya Maisha ya kisasa, ikitoa fursa za afya, kutoa ajira, Maendeleo ya kijamii na umaarufu.
Hata hivyo,wanawake wanakabiliwa na changamoto lukuki wanaposhiriki katika shughuli za michezo mbali mbali nchini na baadhi ya changamoto hizo ni ubaguzi wa kijinsia.
Akizungumza na mwandishi wa Makala hii, Saida Saidi mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya worries anasema moja ya changamoto inayowakabili wachezaji wa kike ni ubaguzi wa kijinsia, kwani mara nyingi wanawake hawapati fursa sawa kama wenzao wanaume katika mashindano mbali mbali .
“ Ukiangalia sisi wachezaji wakike ligi zetu hazina udhamini, hii inatufanya iwe ngumu kujitokeza kwa wingi kuonesha vipaji vyetu kama ilivyo kwa wanaume” anasema mchezaji huyo .
Amesema kuwa, ingawa kuna jitihada mbali mbali za kuboresha nafasi ya mwanamke katika michezo , lakini bado kuna hitajika juhudi za ziada ili kuinua soka la wanawake.
Aidha amesema kuwa, wanawake mara nyingi wanakabiliwa na changamoto za kifedha katika michezo, ukosefu wa wadhamini na rasilimai fedha unawafanya wengi washindwe kudhamini mafunzo na vifaa vyao vya kimichezo.
Nae, mchezaji wa mpira wa miguu kutoka timu ya New Generation Hafidha Juma amesema matarajio ya wanajamii yanaathari kubwa katika maendeleo ya wanawake kwenye michezo.
“Katika jamii nyingi za kiafrika ,kuna mitazamo kwamba wanawake hawawezi kuwa na mafanikio sawa na wanaume katika michezo, hii inawafanya baadhi ya wanawake kujihisi kushindwa hata kabla ya kujaribu” anasema Hafidha.
Amesema kuwa, mitazamo kama hiyo inaweza kuathiri ndoto za Watoto wakike wakiingia katika michezo, wakifikiria ni sehemu ambayo inaweza kuwajiajiri na kuendesha Maisha yao.
Nae, mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya watu wenye ulemavu , Amina Simba, amesema changamoto kubwa inayowakumba timu yao ni ukosefu wa vifaa na maandalizi kwani wana ukosefu mkubwa wa vifaa na mazingira ya kufanyia mazoezi.
Aidha amesema kuwa, hali hiyo inawafanya kuwa kidogo katika mashindani na kuwakatisha tamaa ya kushiriki mashindano mengi ya kimataifa,”Kiukweli hatuna viwanja maalumu vya kufanyia mazoezi na hali hii inatuathiri na kutukatisha tamaa” amesema Amina.
Nae, Kocha wa mpira wa miguu Bi Nasra Juma amesema ni kweli mpira wa wanawake una changamoto ukilinganisha na wanaume.
Amesema kuwa, ni vyema Serikali na mashirika mengine yakajitokeza katika kudhamini mpira wa wanawake ili kusaidia kukuza vipaji vya wachezaji wakike.
"Ni vyema mashirika binafsi yakajitokeza kudhamini ligi za wanawake ili kuinua soka lao, nao kujiajiri kupitia sekta hiyo" amesema Bi Nasra.
Mkurugenzi wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania -TAMWA ZNZ , Dk Mzuri Issa ni mdau mkubwa wa sekta ya michezo kwa maendeleo, wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika, mwaka 2024 alisema ni vyema Watoto wakike kushiriki katika michezo mbali mbali licha ya changamoto zinazowakabili.
Amesema kuwa, changamoto za wanawake katika michezo ni nyingi na zinahitaji juhudi za Pamoja kutoka katika jamii, Serikali na mashirika ya michezo ili kutatuliwa.
“ Ni vyema kila mmoja achukuwe jitihada za kukabiliana na changamoto hizi ili kukuza usawa wa kijinsia katika michezo” ameshauri Dr Mzuri.
HijaMohamed ni mshauri elekezi katika mambo ya kijinsia katika mradi wa michezo kwa Maendeleo unaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani nchini Tanzania ( GIZ) amesema wana malengo ya kujenga viwanja saba vya mpira Unguja na Pemba, ili kuondoa changamoto ya Watoto wa kike kushiriki michezo.
Amesema kuwa, viwanja hivyo vinne vitajengwa Unguja na vitatu vitajengwa Pemba ili kuimarisha sekta ya michezo kwa maendeleo na vijana wengi kuitumia fursa zinazotokana na michezo kujiajiri.
Nae, Katibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar ( ZFF) Hussein Ahmada Vuai amesema sekta ya mpira wa miguu imekuwa na kuimarika kwa kujengwa viwanja vya kisasa ili wachezaji wawe huru kufanya mazoezi na kushiriki michezo.
Amesema kuwa, ni vyema Watoto wakike kuzitumia fursa za michezo kushiriki katika michezo mbali mbali ya ndani na nje ya nchi kwani licha ya changamoto zinazowakabili lakini pia wana fursa nyingi ambazo zinawanufaisha kupitia michezo.
No comments