TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR YAFANYA MKUTANO WA TATHMINI YA UCHAGUZI KISIWANI PEMBA.
Na Said Khamis.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jaji George J. Kazi, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya uwazi, weledi na ushirikiano katika kuimarisha uendeshaji wa Uchaguzi nchini.
Aliyasema hayo wakati wa kufungua Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi uliolenga kutathmini masuala mbali mbali yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025, Mhe. Jaji Kazi alisema wadau wote kwa pamoja wameonesha kuwa mchakato wa Uchaguzi si jukumu la Tume pekee, bali ni wajibu wa jamii nzima,
“Kwa pamoja tumethibitisha kwamba mchakato wa uchaguzi unaweza kuendeshwa kwa uwazi, weledi, ushirikiano na heshima, Uchaguzi si jukumu la Tume pekee, bali ni wajibu wa jamii nzima,” alisema Jaji Kazi
Aidha, alibainisha kuwa msingi uliowekwa katika Uchaguzi wa mwaka huu utabaki kuwa dira na mwanga wa maandalizi ya Chaguzi zijazo, huku akisisitiza dhamira ya Tume kuendeleza mageuzi yenye kujenga imani ya umma katika hatua za Uchaguzi nchini.
Katika mkutano huo, wadau walipongeza juhudi za Tume kwa kuendesha mchakato wa Uchaguzi wa Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025 kwa haki, amani na utulivu, hatua iliyowezesha wananchi kutekeleza haki yao ya kikatiba bila vurugu.
Walisema Tume imeonyesha kwamba kwa ushirikiano, Uchaguzi unaweza kuendeshwa kwa uwazi na kuheshimu misingi ya demokrasia.
Akifunga mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mhe. Jaji Aziza Suwedi, alieleza kuwa hoja zilizotolewa na Wadau hao zitatumika kama nyenzo muhimu katika kuboresha michakato ya Uchaguzi na kuandaa mpango kazi maalum wa mageuzi unaolenga kuongeza ufanisi katika chaguzi zijazo.
Mkutano huo wa Wadau wa Tathmni ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025 umefanyika katika ukumbi wa Makonyo Wilaya ya Chake Chake Pemba na kuhudhuriwa na wadau kutoka Serikalini, Vyama vya Siasa, Vyombo vya Habari, Asasi za Kiraia, Makundi Maalum pamoja na wananchi.

.jpeg)
.jpeg)
No comments