Breaking News

Azam yatua Z'bar yaahidi, kuishangaza Wydad CAF


KIKOSI cha Azam FC, tayari kiko mjini Zanzibar ambapo kimetua moja kwa moja kutoka jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, huku viongozi wa timu hiyo wakiahidi kuishangaza Wydad Casablanca, katika mchezo wa pili Kombe la Shirikisho Afrika, hatua makundi.

Azam, inatarajiwa kucheza mchezo huo, keshokutwa katika Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Hasheem Ibwe, alisema jana baada ya kupoteza mechi dhidi ya AS Maniema Union, Jumapili iliyopita ikiwa ugenini, imejipanga kuhakikisha inashinda mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani, huku wakiwa tayari mjini Zanzibar baada ya kuwasili juzi jioni.

"Ilikuwa ni siku mbaya kwenye mchezo wa kwanza, tulikutana na timu bora sana AS Maniema Union.

"Kuna mchezo mgumu dhidi ya Wydad Casablanca, ukizingatia kuwa wenzetu wameanza vizuri dhidi ya Nairobi City Stars.

"Pia kuna vitu tumejifunza kwenye mchezo ule, tutazidi kuzoea mazingira ya hatua hizi za makundi mechi za kimataifa, tunajipanga na tutafanya vizuri.

"Sisi Azam tunaahidi kuwa katika mchezo wetu wa Ijumaa, tutawashangaza wageni wetu, Wydad Casablanca, wao na wale ambao hawaamini kuwa tunaweza kushinda mchezo huo, hawatoamini kitakachotokea," alisema Ibwe.

Ofisa Habari huyo alisema mara baada ya mchezo ule, hakuna aliyependezwa na matokeo kwani walikuwa na uwezo wa kushinda mchezo kutokana na jinsi walivyoimiliki mechi.

"Tulifanya kila kitu sawa, tulimiliki sana mpira, lakini wenzetu walifanya mashambulizi ya kujibu ambayo yaliwapa mabao yote mawili, hatukupendezwa na kile kilichotokea, kuanzia wachezaji mpaka benchi la ufundi," alisema.

Azam ilipoteza kwa mabao 2-0, huku Wydad Casablanca, ikiitandika Nairobi City Stars, mabao 3-0, katika mechi za Kundi B, zilizochezwa mwishoni mwa wiki.


No comments