WANAWAKE WATAKIWA KUSHIKANA MIKONO KUTIMIZA MALENGO NAFASI ZA UONGOZI.
WANAWAKE nchini wametakiwa kuweka pembeni tofauti zao za kisiasa na badala yake kushirikiana, kuungana na kusaidiana katika harakati za maendeleo na uongozi ili kuongeza ushiriki wao katika nafasi mbalimbali za maamuzi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), Nairat Abdulla Ali, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu wanawake na uongozi yaliyowashirikisha madiwani wanawake pamoja na waratibu wa shehia wanawake.
Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa TAMWA uliopo Tunguu na ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuwawezesha Wanawake katika Uongozi na Siasa (SWIL), unaolenga kuimarisha uwezo wa wanawake kushiriki kikamilifu katika masuala ya uongozi na maendeleo.
Nairat alisema kuwa wanawake wanapaswa kutambua kuwa licha ya tofauti zao za vyama vya siasa, wanakabiliwa na changamoto zinazofanana, hivyo ni muhimu kushirikiana ili kufanikisha malengo yao ya pamoja.
Alieleza kuwa umoja na mshikamano miongoni mwa wanawake ni nyenzo muhimu itakayowasaidia kujenga ushawishi mkubwa zaidi katika ngazi mbalimbali za maamuzi na kuongeza idadi ya wanawake wanaoshika nafasi za juu za uongozi.
Aidha, alisema pamoja na wanawake kuwa wengi katika jamii, bado uwakilishi wao katika nafasi za uongozi haujafikia kiwango kinachoridhisha, hali inayohitaji juhudi za makusudi ili kubadilika.
Alifafanua kuwa kwa sasa wanawake madiwani ni asilimia 24 pekee, kiwango ambacho hakilingani na idadi ya wanawake waliopo katika jamii na mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wanawake kuendelea kupeana nguvu, kuhamasishana na kujiamini ili idadi yao iongezeke zaidi katika uchaguzi mkuu ujao na katika nafasi nyingine za uongozi.
Nairat alisema mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kwa lengo la kuwajengea uwezo madiwani wanawake na waratibu wa shehia ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kujiandaa vyema kwa fursa zijazo za uongozi.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia washiriki kuelewa kwa kina namna ya kuwakilisha wananchi, kushughulikia changamoto za jamii na kujenga mahusiano bora na makundi mbalimbali katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa SWIL kutoka TAMWA ZNZ, Sabrina Yussuf Mwintanga, alisema taasisi hiyo itaendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wanawake kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Alisema uwekezaji katika mafunzo na ujenzi wa uwezo kwa wanawake ni hatua muhimu katika kuhakikisha wanapata nafasi sawa za kushiriki katika mchakato wa maamuzi na maendeleo ya nchi.
Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Imane Duwe, alisema kiongozi bora anatakiwa kuwa na uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi pamoja na kuhamasisha maendeleo katika maeneo yake.
Alisema kiongozi ni mtu anayetoa mwelekeo, huonyesha dira ya maendeleo na huwahamasisha wengine kufikia malengo yaliyowekwa kwa manufaa ya jamii.
Imane alibainisha kuwa viongozi wanawake wanapaswa kuwa wabunifu, wawajibikaji, wenye kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi na kuhakikisha uwazi katika utoaji wa huduma kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Diwani wa Wadi ya Mwanakwerekwe, Fatma Jabu, alisema wanawake bado wanakumbana na changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kufikia malengo yao ya uongozi.
Alieleza kuwa mfumo dume bado ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyowarudisha nyuma wanawake wengi katika kugombea na kushika nafasi za maamuzi, licha ya uwezo walionao.
Fatma aliishukuru TAMWA ZNZ kwa kuandaa mafunzo mbalimbali akisema kuwa yamewapa maarifa, ujasiri na uthubutu wa kujitokeza kugombea na kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Nae Diwani wa Wadi ya Kihinani, Bahati Ali Rashid, aliwataka wanawake kutokata tamaa, kujiamini na kutumia fursa zilizopo ili kufanikisha ndoto zao za uongozi.
No comments